11/02/2024
Mpenzi Azimio
Hivi punde nimekuwaza tena nikisherehekea siku yako ya kuzaliwa ya miaka 57. Kuna maswali yamekuwa yananikera sana na bado sijapata majibu ya kuridhisha.
Nafikiri ninaelewa vema – au ninafikiri ninaelewa – mazingira ya kuzaliwa kwako. Pia kwa kiasi fulani nimeanza kusuka hatua kwa hatua jinsi ulivyouliwa. Lakini bado sielewi uhusiano wako na mlezi wako; Mzee yule ambaye tulizoveya kumuiita Mwalimu. Siku hizi anaitwa Baba wa Taifa. Labda baba ni hadhi ya juu kuliko Mwalimu lakini sio kwangu. Mwalimu anakufundisha wakati wa uhai wake na hata baada ya kuondoka. Lakini baba akiondoka unamsahau baada ya siku chache za maombolezo. Zaidi zaidi unamsalia kila mwaka tarehe ya kifo chake. Ah! Niwie radhi tabia yangu ya kuhamahama kutoka mada yenyewe.
Nilichokuwa nasema uhusiano wa Mwalimu na wewe na jinsi alivyokuwa anakuona bado sijaelewa vizuri. Je uhusiano huo ulisimama kwenye msingi imara wa kisiasa au ulikuwa wa kigeugeu kutokana na hali halisi ya siasa?
Sijui. Sinajibu. Nimuulize nani? Wewe haupo. Na hao ambao wanajiita makamaradi zangu hawana interest. Wako bizi na shughuli zao zingine.
Mara ya mwisho akikuzungumzia Mwalimu alisema hatakusahau na kwamba yeye alikuwa anatembea na vitabu viwili Biblia na Azimio. Sasa je alikuweka daraja sawa na Biblia? Je alianza kukuabudu? Je wewe mtoto mwenye utambulisho wa kisiasa thabiti uligeuka kuwa Nabii?
Nahisi usingizi. Nitaendelea wiki ijayo.
Wako
Issa
| Barua ya Wiki ya 11 Feb 2024 |



Leave a comment