3 bARuA YA KILA WIKI KWA MPENZI WANGU AZIMIO

25/02/2024

Mpenzi Azimio

Duh! Ujio wako juzi uliniacha hoi. Hasira zako zilivuka mipaka ya kistaarabu. Ukanikaripia; ukanikemea. Ukaniumiza sana. ‘We fedhuli we. Mimi sina muda na hizi hisia mufilisi za mapenzi …. Kwani hukuwa na chochote cha kusema juu ya mapinduzu … ukanipotezea muda bure!’ Wala hukunipa nafasi ya kujitetea. Ghafla ukaondoka. Ghafla nikaamka nikiwa ninavuja jasho hovyo. Hata mama watoto kashtuka.  Alitaka kunipeleka hospitali. 

Hilo la uhusiano kati ya mapenzi na mapinduzi nitalizungumzia siku nyingine ukiwa umetulia. Nirejee kwenye hoja zangu. 

Katika miaka ya 90 hivi, Mwalimu alianza kupoteza imani na chama chake, CCM. Hakuwana uhakika kwamba CCM na viongozi wenzake wataendeleza tena mtazamo wa kijamaa. Alihisi kwamba vivutio vya kibepari vilianza kutamanisha baadhi ya viongozi wa chama na serikali. Wakishawishiwa na ushauri na maono ya “wafadhili” wa kibeberu, wakaanza kuchukua hatua za kurejesha mfumo wa kibepari. Na katika mwelekeo huohuo wakalegeza na hatimaye kufuta kabisa miiko ya uongozi tulijiwekea katika Azimio la Arusha. 

Isitoshe, mazingira ya kimataifa yalibadilika sana. Ubeberu na ubepari ukarejea kwa kishindo. Itikadi ya ujamaa ikabezwa. Nchi za kijamaa hususan Soviet Union zikaanza kusambaratika. Ubeberu na ubepari ukaongeza propaganda zao mara dufu – kukashifu ujamaa na kuonyesha uzuri wa ubepari. Mazingira hayakuwa rafiki. Wajamaa walijikuta wanapoteza matumaini; wengine wakasalimu amri, wengine wakajigeuka kuwa wapigadebe wa ubeberu; wengine wakajistiri binafsi kwa kuamini dini. Wachache waliobaki na mtazamo wao wa kijamaa wakauficha ficha kiasi cha kuathirika kiafya na hata kisaikologia. 

Mwalimu mwenyewe aliwahi kuteta katika moja ya mkutano wa kimataifa huko Arusha kwamba kuzungumza tena ujamaa nyakati zile ingekuwa upumbavu – ndio maana alikuwa ananong’ona tu!  

Kwa hivyo, mpenzi wangu, hoja yangu ni kwamba hii ya kutumia misamiati ya kidini dini akiwa anazungumza Azimio ilikuwa ni ishara kwamba Mwalimu ‘alisalimu amri’ katika mapambano yake ya kisiasa ya kujenga nchi ya kijamaa. Nakumbuka sana aliwahi kutenganisha sera ya kujitegemea na ujamaa akiwaambia viongozi wenzake kitu kama ‘mnaweza kuuachana na ujamaa mkitaka lakini msiachane na sera ya kujitegemea.’ Mimi binafsi nilishanga Mwalimu akitenganisha ujamaa na kujitegemea. Kwa kizazi changu ujamaa na kujitegemea zilikuwa kama pacha. Huwezi ukajitegemea kama nchi bila kuwa na mtazamo na mwelekeo wa kujenga ujamaa na huwezi kujenga ujamaa bila ya kujitegemea. Sasa, kweli, Mwalimu aliamini kwa dhati kwamba nchi inaweza kujitegemea bila ujamaa au mahubiri yake hayo yalikuwa tu kujifarijisha yeye binafsi? 

Sasa kama kuna ukweli wowote katika hoja yangu kwamba Mwalimu ‘alisalimu amri’ , sinabudi nithibitishe kwa kuchambua historia ya kisiasa ( political history) ya kutenguliwa kwa Azimio la Arusha. Mabadiliko katika mwelekeo wa Mwalimu haukutokea ghafla bila sababu au mantiki; yalikuwa na chanzo chake katika historia na siasa ya miongo ya 80 na 90. 

Nitaendelea kuchambua historia na siasa za 80 na 90 katika barua zangu zijazo. 

Wasalaam

Issa

One response to “3 bARuA YA KILA WIKI KWA MPENZI WANGU AZIMIO”

  1. Asante sana Ndugu ISSA .nazidi kujifunza kuhusu mapambano ya Mwal katika kujenga UJAMAA je kama Mwal alisalimu amri katika falsafa yake ya UJAMAA Je sera za kijamaa zinaweza tekelezwa tena??

    Like

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags