17/03/2024
Mpendwa Azimio
Katika kipindi chake cha pili (1987-1990) cha unenyekiti wa Chama baada ya kung’taku madaraka ya serikali, Mwalimu alishuhudia matukio matatu muhimu ambayo inawezekena yaliyomsukuma kujiuzulu uenyekiti wake kabla ya kumalizika kwa kipindi chake.
Moja ni kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Kusini (South Commission). Tume iliteuliwa kutokana na pendekezo la hayati Robert Mugabe akiwa rais wa Zimbabwe. Hoja ilikuwa kuwa na Tume ambayo itachunguza hali ya dunia, hususan mgawanyiko kati ya nchi tajiri zilizoendelea za Kaskazini na nchi maskini zinazoendelea za Kusini, kwa mtazamo na maslahi ya Nchi za Kusini na kutoa mapendekezo na ushauri jinsi ya kujinusua kutokana na hali duni. Kabla ya hiyo, kulikuwa na Tume mbili, ile ya Willy Brandt, rais mstaafu wa Ujerumani Magharibi na ya Gro Harlem Bruntland, Waziri Mkuu mstaafu wa Norway, zote zikiangalia mgawanyiko huo lakini kwa mtazamo wa nchi za Kaskazini.
Kwa miaka takriban mitatu Mwalimu alitembelea nchi nyingi za Kusini au dunia ya tatu; kukutana na viongozi na wasomi wa nchi hizo na kuwa na mijadala nao. Bila shaka jambo moja Mwalimu asingekosa kujifunza ni kwamba siasa na mitazamo ya nchi hizi, nyingi zilizopitia utawala wa kikoloni, zilibadilika sana. Lile viguvugu la ukombozi na ujivunio wa uhuru iliyomotisha watu na hata serikali katika miongo ya 60 na 70 ulififia kana kwamba baadhi ya nchi zilikuwa tayari kukubali tu ukandamizaji wa kiuchumi wa nchi za Kaskazini badala ya kuendelea na mapambano dhidhi ya uhusiano wa kimataifa usio wa haki.
Hata katika Tume yake walikuwepo wajumbe akiwemo Katibu wa Tume Manmohan Singh ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa India, waliegemea zaidi kwenye mtazamo wa uliberali mambolea. Wajumbe wa Tume yenyewe waligawanyika. Lakini Mwalimu akiwa mtu mwenye msimamo wa kati aliweza kuhakikisha kwamba hatimaye wanatoa ripoti iliyokuwa inakubalika kwa wote. Matokeo yake ni ripoti ya Tume ya Nyerere haikuwa na ukali wa Nyerere. Ilikuwa ni ‘compromise report’ – kaaina ka maelewano kati ya wajumbe wa mrengo wa kushoto na mrengo wa kulia, Mwalimu mwenyewe akiwa katikati kama referee badala ya mchezaji.
Jambo la pili kutokea ni kuwa na mvutano (tension) kati ya Chama chini ya Mwalimu na serikali chini ya Mwinyi. Kwa mfano, kamati kuu (KK) ilikuwa inatoa mwongozo kwa serikali kujitahadhari katika majadaliano na Shirika la Dunia la Fedha IMF. KK ilikuwa ina weka kikomo cha ushushaji wa thamani ya shilingi. Lakini kila mara serikali ilikuwa inakubaliana na IMF kuvuka kikomo kilichowekwa na KK kwa hoja kwamba IMF haikuwa tayari kulegeza msimamo wake.
Mwishoni mwa miaka ya 80 kulikuwa na matamko ya baadhi ya mawaziri wa serikali yakiashiria ubinafsishaji wa baadhi ya mashirika ya umma. Vijana wa Youth League wa Chama walipitisha azimio katika semina yao wakionya dhidhi ya ubinafsishaji wakisema utahatarisha ujamaa. Hata hivyo Mwalimu kakaa kimya. Hakuunga mkono vijana. Inaelekea alianza kukataa tamaa.
Baada ya serikali ya awamu ya pili kulegeza masharti ya biashara na uingizaji wa hela za kigeni, baadhi ya viongozi wa serikali walianza kujishughulisha na biashara na uwekezaji katika usafiri n.k. Masharti ya uongozi bado yalikuwepo lakini serikali ilifumbia macho. Wananchi kwa upande wao walikuwa wanashuhudia hayo. Chama kikaanza kupoteza heshima yake. Nyakati hizo ndio majina ya kejeli yakajitokeza: CCM – Chukua Chako Mapema, Chama Cha Majangili n.k
Jambo la tatu na la muhimu ni mageuzi makubwa yaliyotokea katika kambi ya nchi za kijamaa huko Ulaya. Mikhail Gorbachev akachukua sukani ya Chama cha Kikomunisti cha Muungano wa Nchi za Kijamaa (Union of Soviet Socialist Repulics, USSR) mnamo 1985. Akaanza kufanya mageuzi katika chama na serikali chini ya kauli mbiu glasnot (uwazi) na perestoika (ulegezaji wa uthibiti wa chama). Mageuzi yakashika kasi. Mabadaliko makubwa ya serikali yakaanza kutokea katika nchi za kijamaa za Ulaya Mashariki. Ukuta wa Berlin uliokuwa unatenganisha Ujerumani Masharki (katika kambi ya ujamma) na Ujerumani Magharibi (katika kambi ya ubepari) ukabomolewa mnamo 1989. Huu ukawa mwanzo wa mwisho wa nchi za Ulaya za kijamaa. Hatimaye USSR yenyewe na nchi nyingi za Ulaya Mashariki zikasambaratika.
Matokea ya hayo yote na mageuzi makubwa katika hali ya kimataifa bila shaka yalimfanya Mwalimu afikirie hatma ya Ujamma nchini kwake na uongozi wake wa chama ambacho kilikuwa kishaonyesha mrengo wake wa kulia chini ya Mzee Mwinyi. Kwa Mwalimu umoja wa nchi ulikuwa muhimu zaidi kuliko nchi kuwa nchi ya kijamaa. Ni vema kuelewa fikra za Mwalimu. Hofu ya nchi kusambaratika ilikuwa inamsumbua sana. Kwake umoja wa kitaifa ulikuwa muhimu zaidi kuliko itikadi ya chama chake. Hakutaka yaliyokuwa yanatokea katika nchi za Ulaya za kijamaa itokee nchini kwake.
Kafanya uamuzi mgumu. Kamuachia Mwinyi ngazi ya uenyeketi kabla ya kumaliza kipindi chake na kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi.
Mwalimu kaondoka. Mwinyi kapumua.
Mzee Mwinyi kashinda urais kwa kushindo. Kajiamini. Kashika hatamu ya serikali na chama kuongoza kama yeye Mwinyi sio tena kama kivuli cha Mwalimu.
Nitaendelea na simulizi ya Mwalimu na Mwinyi katika barua ijayo.
Wasalaam
Issa Shivji



Leave a comment