7/04/2024
Mpendwa Azimio
Nitaendelea kukusumbua na barua zangu mpaka nimemalizi simulizi ya awamu zote. Niwie radhi. (Inalekea wajukuu wako wameanza kuzisoma na kuzipenda barua hizi). Najizuia kuingiza neno la upendo kwa sababu inaelekea umenisusia au labda unasubiri nimalize simulizi zangu. Vyovyote vile namiss sana tabasamu zako.
***
Awamu ya nne chini ya Mhe. Kikwete ilikuwa kuvuna matunda matamu kwa walalaheri na matunda machungu kwa walalahoi. Baadhi yetu tulitabiri na kutoa angalizo kwamba tukikumbatia soko huria bila uthibiti wowote na tukibinafsisha holela mashirika ya umma, walalahoi wataathirika sana. Kwanza, watakosa ajira. Idadi ya wafanyakazi wasiona ajira itaongezeka. Ikatokea. Tulisema soko huria ni njia thabiti ya kugawanya watu; ya kuoongeza pasuko ya jamii kati ya walionacho na wasionacho. Ikatokea. Tulisema serikali ikiondoa ruzuku kwa vyakula, gharama ya maisha itaongezeka mara dufu. Ikatokea. Tulisema tukibidhaaifisha huduma muhimu za kijamii – elimu, afya, maji safi, umeme n.k., – ujinga na ugonjwa wa watoto wa walalahoi yataongezeka. Afya zao zitaathirika. Ikatokea.
Waliokosa kazi iliwabidii wafanye kibarua au kazi zisizona staha kwa kipato duni. Ikatokea. Badala ya kuiona sekta isiyorasmi (informal sector) dalili ya ugonjwa, serikali na wasemaji wake walishangilia ukuuaji wa sekta isiyorasmi eti ishara ya watu kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wa wakulima na wafugaji vijijini, maisha hayakuwa na uhakika, wazalishaji wadogo daima wakihofia usalama wa ardhi yao. Miradi mikubwa kama SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania) ikapewa kipau mbele. Wawekezaji wa mradi huo walikuwa mashirika makubwa ya kilimo ( agribusiness) lengo lao likiwa kuingiza wakulima katika mnyororo wa biashara ya kimataifa ambao unatawaliwa na mabepari papa wakibuni kila uchao njia mpya za kunyonya jasho la wazalishaji. Kwa upande wa serikali kisingizio kikawa kuongeza tija katika kilimo kwa kukigeuza kuwa kilimo cha biashara bila kujali kwamba hao wakulima wangekosa ardhi kulima chakula chao na kuwa wategemezi wa misaada.
Haya ndio yalikuwa nilichoiita matunda machungu “walichovuna” wavujajasho (wakulima na wafanyakazi) kutoka uliberali mamboleo. Je ilikuwaje kwa upande wa walalaheri (watawala, watendaji wakuu serikalini, wafanyabiashara na matajiri wengine)? Uliberali mamboleo ulifunguwa milango mipya kwa hao wenye uchu wa kujitajirisha haraka haraka kwa njia halali au haramu. Ubadhirifu na rushwa iliongezeka. Kila uchao tulikuwa tunasikia ufichuaji wa kashfa mpya na ufisadi. Nidhamu katika taasisi za serikali ilishuka. Huduma mbalimbali kutoka serikali ikawa na bei (yaani haikupatikana bila kutoa hongo). Ubabe wa wapigadili ukavuka mipaka. Chama kikapoteza uwezo wake mdogo uliyobaki kudhibiti serikali na wakuu wa taasisi wa serikali wakapoteza uhalali wa kudhibiti watendaji chini yao. Ungetegemea je maadili kutoka mtendaji wa ngazi ya chini wakati watendaji wa ngazi ya juu wenyewe walikuwa wapigadili?
Pamoja na matukio hasi niliyosimulia hapo juu, hatunabudi tukiri kwamba chini ya urais wa Mhe. Kikwete uhuru wa mawazo uliongezeka. Mhe Kikwete hakua na hulka ya kuwakandamiza au kuwalipiza kisasi waliompinga. Vyama vya upinzani vilifanya shughuli zao bila kubughudhiwa na vyombo vya mabavu. Pamoja na upana wa uhuru wa mawazo, kama haikutokea ukosoaji wa dhati wa mfumo wa uliberali mamboleo kutoka kwa wanazuoni na vyombo vya habari visivyo vya serikali ni kwa sababu wengi wa wanazuoni wenyewe wakawa wapigadebe wa uliberali mamboleo. Na vyombo vya habari walikuwa wanalinda maslahi yao. Hata hivyo walikuwepo wachache walikuwa na ujasiri wa kufichua ufisadi. Baadhi ya wanazuoni, ingawa wachache, waliandika kukosoa kilichokuwa kinaendelea. Baadhi ya mashirika yasiyo ya serikali walikuwa wanafanya kazi nzuri ya kutetea haki za wanyonge. Lakini walikuwa wachache.
Ukweli ni kwamba athari kubwa ya uliberali mamboleo ilikuwa kushawishi ubinafsi kupita kiasi. Hulka ya kutokujali, ya kutokuguswa na dhiki ya binadamu mwenzako, ulienea sana hasa katika matabaka ya vibwenyeye. Tulishuhudia ufifiaji wa utamaduni wa kijamii takriban katika nchi zote zilizokumbatia uliberali mamboleo. Margaret Thatcher, Waziri Mkuu wa Uingereza na mpigadebe maarufu wa uliberali mamboleo, aliwahi kusema: Jamii! Jamii gani. Hakuna kitu kama jamii – kuna watu binafsi tu. (Society! What society? There is no such thing as society. There are only individuals.)
***
Uchaguzi mkuu wa 2015 ulikuwa changamoto kwa CCM. Uongozi wa juu wa Chama (waliokuwepo na waliostaafu) walihisi, ingawa hawakusema hadharani, kwamba wananchi walianza kupoteza imani na CCM na uongozi wake. Isitoshe, katika kipindi cha Mhe. Kikwete, Katibu Mkuu wa Chadema Dr Slaa alipaza sauti nchi nzima akitangaza majina ya mafisadi wa CCM na dhambi zao. Kulikuwa na hatari ya CCM kushindwa katika uchaguzi. Walihitaji kumsimasha mtu ambaye hakuwa na doa; mtu safi; mtendaji na mfuatiliaji. Uteuzi wao ukaangukia kwa hayati Magufuli.
Magufuli hakukulia katika Chama wala hakuwa kiongozi katika Chama. Kwa hivyo, wapigakura labda wangemamini zaidi kuliko viongozi waliokuwa wanajulikana na dhambi zao zilikuwa gumzo vijiweni. Hatimaye Magufuli kashinda lakini kwa kura chache (58%) kuliko marais wote waliomtangulia.
Awamu ya tano chini ya hayati Magufuli ilikuwa ya kipekee; tofauti kabisa na awamu zote zilizotangulia ikiwemo awamu ya Mwalimu Nyerere. Nitaisimulia katika barua yangu ijayo.
Wasalaam
Issa



Leave a comment