10 barua ya kila wiki kwa mpendwa wangu azimio

14/04/2024

Mpendwa Azimio

Wananchi walichoshwa na hali ya kiholela ya miaka kumi ya awamu ya nne. Kiuchumi, kwa walio wengi, maisha yalikuwa magumu. Walipoteza matumaini ya kesho. Hawakuona watapataje ahueni. Wakimulika chama tawala au vyama vya upinzani na viongozi wake walihisi wengi wao walikuwa wakitetea maslahi yao binafsi. “Viongozi” walipoteza hisia za uchungu wa maisha ya walalahoi. 

Katika hali kama hii watu wengi huwahawaoni mahali pa kugeukia isipokuwa dini zao, makabila yao au koo zao. Wengine wana tafuta ahueni hata katika ushirikina. Hisia za kitaifa au utambulisho wa kitaifa unapoteza maana na mvuto.  Taifa halina cha kutoa, si matumaini sikitoweo. Kunakuwa na ombwe la kijamii.  Kinachobaki ni kusubiri masiha atokee kuwakomboa, kujaza ombwe hilo. Kwa walalahoi wengi na wengine waliopotezaimani na viongozi na siasa, hayati Magufuli alijaza ombwe hilo. 

Juu ya jambo hili, naamini kwa dhati kabisa kuwa Magufuli alijiona kama masiha aliyetumwa na Mungu kujakuokoa wanyonge. Yeye mwenyewe alikuwa akisema hivyo mara kwa mara. Sidhani kuwa Magufuli alikuwa mdanganyifu. Aliamini kabisa katika mission (wito) wake, na walalalahoi pia walimuamini. Ukijiona kwamba wewe ni mkombozi, unafanya kazi ya Mungu, mikono yako haifungwi na sheria wala tamaduni za kisiasa. Mtu mwenye hulka hii hawezi kuelewa uwajibikaji kwa wananchi au wawakilishi wa wananchi. Yeye si mwakilishi mkuu tu  bali ni mwakilishi wa pekee wa wananchi. Wengine wote chini yake ni watendaji wa kuambiwa, kuamrishwa na kusimamiwa. 

Ndivyo hali ilivyokuwa chini ya utawala wa rais Magufuli. Nirudie kusisitiza; Magufuli hakuwa tapeli wala mdanganyifu. Alichokuwa akifanya, alikifanya kwa nia nzuri. Suali ni alifanya nini.

Kwanza, alirejesha nidhamu katika utumishi wa umma kwa njia mbalimbali ikiwemo kukaripia na kuwadhalalisha watendaji wakuu hadharani, hata kuwafukuza bila kujali kanuni za utumishi wa umma. 

 Pili, alipunguza sana hongo na rushwa, hasa ya wazi wazi, katika ngazi ya kati na chini ya utumishi wa umma. Hata waadui wake wanakiri jambo hili. 

Tatu, alipunguza kwa kiasi kikubwa masumbufu kwa watu wa chini, hususan wamachinga na wafanyabiashara wadogo. Katika ofisi na taasisi za serikalikama hospitali, ofisi za ardhi, na wizarambalimbali, mapokezi ya  wananchi yalibadilika yakawa mazuri na yaheshima. Hakuna shaka alikuwa kipenzi cha walalahoi. Na pia hakuna shaka mabwanyenye wa ndani na nje ya serikali hawakumpenda. 

Nne, aliweza kuongeza makusanyo yakodi kwa njia za kisheria na nje ya sheria, pamoja na kuwatisha wafanyabiashara wakubwa na hata kuwatia ndani. Pleabargaining – yaani mfungwa kutoa hela kiasi kikubwa kwa ahadi ya kuachiliwa huru – aliifanya njia moja wapo ya serikali kujipatia fedha. 

Tano, aliwekeza kwenye miradi mikubwa – SGR, bwawa la Nyerere, ujenzi wa miundo mbinu –  kutoka fedha za kodi na mikopo kutoka mabenki binafsi kwa riba kubwa. Bahati mbaya, ni vigumu kupata takwimu. Wakati wa Magufuli ilipitishwa sheria kuwa mtu yeyote akitoa takwimu zozote bila ya idhini ya mamlaka ya serikali inayohusika na takwimu lilikuwa kosa la jinai. 

Sita, aliyatikisha makumpuni makubwa ya madini yaliyokuwa yanasafirisha rasilimali za nchi nje ya nchi kwa njia  zisizo halali. Nchi za kibeberu zenye makampuni haya zilimchukia sana Magufuli. 

Saba, alisitisha mradi wa SAGCOT akihisi sio kwa faida ya nchi ingawa hakuwa na mtazamo  madhubuti wa kuboresha kilimo. 

Kwa jumla, hatua hizi na nyingine, na maaumuzi ya papo hapo – yakiwemo ya kutoa zawadi ( kama wafalme wa kale) au kuchangisha hela kwa ajili ya mama ntilie au mjane  – ilimfanya apendwe na watu wa hali ya chini. Alikuwa msimamizi mzuri lakini haina maana kuwa alikuwa kiongozi mahiri mwenye kipaji na uelewa wa jamii yake na hali ya dunia.  

Hatuna budi pia tuangalie upande wa pili ya sarafu. 

Moja, rais Magufuli alipenda sana kusifiwa. Kila binadamu anapenda kusifiwa lakini Magufuli alipita kiasi. Sifa hii kwa Mkuu wa nchi ina athari mbaya. Viongozi waliomzingira Magufuli walitumia udhaifu wake huo kujipendekeza. Walaghai walijipenyeza katika nafasi nyeti za kisiasa wakipewa dhamana na vyeo ambavyo hawakustahili. Mbaya zaidi, watendaji na washauri walimdanganya kwa kumumwagia sifa tele badala ya kumueleza ukweli. Wimbo wa kila kitu kizuri ni huruma ya Mkuu, ulianza wakati wa awamu ya tano. Darasa likijengwakijijini ni zawadi au ni kwa rehema ya mheshimiwa. Barabara ya kijiji ikiboreshwa kwa nguvu za wanakijiji anayepewa shukrani ni rais. Safari moja hayati Mzee Mkapa aliukosoa mtindo huu. Sidhani Magufuli alipendezwa sana na ukosoaji wa Mkapa, ingawa haukuwa wa moja kwa moja. 

Pili, kwa hulka hiyo hiyo, rais Magufuli alikuwa haushauriki, hata na wataalamwake. Kwa mfano, alipuuza maandiko ya kitaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu athari hasi za kimazingira ambazo zingeweza kusababishwa na mradi wa bwawa la Nyerere. 

Pia alipuuza ugonjwa wa UVIKO-19 kiasi cha kuwafukuza wakuu wa maabara ya serikali. Inawezekena vifo viliyotokea katika janga hili visingetokea kama dawaza chanjo zingenunuliwa na watuwakapata chanjo mapema. 

Tatu, hayati Magufuli hakupenda kabisa kukosolewa na hata watu wenye nia njema. Yeye aliona kila mkosoaji ni mpinzani. Kwa kiasi fulani rais Magufuli alikuwa anahofia sana usalama wake binafsi. Vyama vya siasa na baadhi ya viongozi wake waliathirika. Wengine walipotea au kutekwa nyara na watu wasiojulikana, jambo ambalo halikuwahi kutokea nchini upande wa Tanzania Bara. 

Nne, uhuru wa kutoa mawazo na uhuru wa fikra (freedom of speech) na uhuru wa vyombo vya mawasaliano ulibanwa sana. Sio tu wanahabari lakini hata wanazuoni waliishi kwa hofu wakifungwa midomo kwa vitisho, ama vya moja kwa moja au kupitia ujumbe. 

Tano, ingawa Magufuli alihisi kwamba utajiri wa nchi ulikuwa unanyonywa na makampuni ya kibeberu, hakuwa na uelewa mpana wa mfumo wa kimataifa wa ubeberu. Haikumjia akilini kuandaawananchi wake katika mapambano ya uchumi dhidi ya ubeberu na vibaraka wao wa ndani. Yaani mwelekeo mzima wa ushirikishwaji wa wananchi katika uendeshaji wa nchi ulikuwa nje ya fikra zake. Ndiyo kusema, utetezi wa wanyonge ulikuwa kutoka juu wakati wanyonge wenyewe wakiwekwa kando katika utetezi wao. Ni kana kwamba wanyonge walikabidhi nguvu zao na uwezo wao wa kupambana kwa mheshimiwa. 

Mwishoni, lazima tukiri,  chini ya utawala wa rais Magufuli vyombo vya mabavu – km polisi – vilipewa na kujipatia uhuru usiona mipaka bila kudhibitiwa na vyombo na viongozi wa siasa. Hii ni hatari kwa nchi yoyote. Usimamizi na uthibiti wa vyombo vya mabavu ni kazi na jukumu la vyombo na viongozi wa siasa. 

Hatimaye uchaguzi mkuu wa 2020 ni dalili tosha ya hayati kutokujali demokrasia na ushirikishwaji wa wananchi. Ni kweli, tumekosoa na tuendelee kukosoa  mfumo wa demokrasia ya kiberali na upungufu wake,  lakini uchaguzi huru na wa haki ni nguzo muhimu ya ushirikishwaji wa wananchi na haiwezi kuepukwa katika mfumo wowote ule unaodai ni wa kidemokrasia. Ni wazi rais Magufuli angeshinda, na CCM kingepata viti vingi bungeni. Lakini je, Magufuli angeshinda kwa asilimia 80 na wapinzani wakakosakaribu viti vyote bungeni, kama matokeoyasingeingiliwa? Moja ya matokeo yakuchakachuliwa kwa uchaguzi ilikuwa idadi kubwa ya wasiostahili waliojipenyezaau waliopenyezwa katika vyombo vya uwakilishi, jambo lilioathiri ubora naumakini wa vyombo vya uwakilishi.  

Ni muhimu kwetu kutokujitumbukiza kwenye propaganda ama ya kumsifu hayati kupita kiasi au kufikiri kuwa yeye nishetani aliyeharibu kila kitu. Ili kujifunza na kupata masomo kutokana na historia yetu, hatuna budi kuzingatia uhalisia (reality) na methodolojia ya uchambuzi tunduizi wa kisayansi. Kamwe  sisi wanazuoni tusijigeuke kuwa wapiga debe wa utawala wowote ule. 

Wasalaam

Issa

4 responses to “10 barua ya kila wiki kwa mpendwa wangu azimio”

  1. asante sana mwalimu Kwa Barua hii.Nimekuoata vizuri sana,tukisifia mazuri tuwakumbushe na mabaya yake

    Like

  2. Asante kwa maarifa makini

    Like

  3. Asante sana Prof Kwa Ujumbe mzuri Hakika Kila Utawala unamazuri yake na madhaifu au mabaya yake

    Like

  4. Asante sana

    Like

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags