12 barua ya kila wiki kwa mpendwa wangu azimio

28/04/2024

Mpendwa Azimio

Nilifurahi sana uliponitembelea ndotoni. Ulikuwa na nyuso ya tabasamu. Ukanikalisha kwenye stuli. Ukakunja nyuso. Ukaanza kwa ukali:

‘Ewe Issa

Mwana wa Mariamu

Achana na mapenzi

Shikamana na itikadi

Itikadi ya wavujajasho

Mkombozi wa walalahoi. 

Usijizoweshe kuvumilia upumbavu

Wa walalaheri na wasomi wao

Pambana nao kwa nguvu ya hoja

Kwa mkakati uliobora

Kwa ujasiri usioterereka. 

 Kamwe usijidanganye

Tabaka-nyonyaji si rafiki

Hakuna maelewano nalo

Kuna mapambano tu.’

Duh! Jasho likaanza kunitiririka. Mwili mzima ukaanza kutetemeka. Sikudiriki kuomba maji wala tawlo la kupangusia.  Nilishindwa kutofautisha. Hili lilikuwa lawama au angalizo. 

Sasa ukaendelea kwa utulivu kwa sauti yako nyororo.  

‘Baadhi ya barua zako zilikuwa nzuri’. Sikuweza kuficha tabasamu yangu. ‘Lakini baadhi ya hoja zako lazima ujikosoe. Nitakusaidia. 

‘Kwa mfano, umempamba mlezi wangu Mwalimu Nyerere kupita kiasi. Mwalimu hakuwa malaika. Alikuwa binadamu kama sisi. Lakini alikuwa zaidi ya binadamu wa kawaida. 

Alikuwa Mkuu wa nchi: Mkuu wa dola na kama Mkuu wa dola alikuwa in-charge wa vyombo vya mabavu. Tena yeye mwenyewe aliwakumbushia hilo huko ukumbi wa Nkrumah. Si mlionja mabavu ya FFU 1978! 

Mwalimu alifanya makosa. Mengi kutokana na mazingira ya wakati ule lakini mengine ni kutokana na mtazamo wake yeye mwenyewe. 

Kati ya 1971 na 1974, kulikuwa na vuguvugu la wafanyakazi viwandani. Wakaanza na migomo. Migomo ilikuwa marufuku. Haraka wakabuni mkakati mwingine. Wakaanza kuwafungia menejimenti katili nje ( locking out management). Hili lilikuwa jipya. Huwa muajiri ndio anawa lock-out wafanyakazi. Menejimenti nje, wafanyakazi ndani. Wakaendelea kuzalisha bila menejimenti. Sasa kama wafanyakazi wanaweza kuzalisha wao wenyewe bila menejimenti, bila muajiri, kwa nini wao wenyewe wasimiliki kiwanda! Ndio mantiki waliofuata. Wakatwaa kiwanda. Duh!  Hili haliwezi kuvumiliwa na mabepari. 

Katika vuguvugu lao kila mara wafanyakazi walikuwa wanamnukuu Mwalimu. Walitumia hasa maneno ya mdogo wangu Mwongozo aliyezaliwa 1971. Silaha yao ya kujikinga ilikuwa ibara mojawapo ya Mwongozo almaarufu kama Ibara ya 15 iliyokataza unyapara kazini. 

Naam! Vuguvugu hili lilikuwa la kihistoria. Halijawahi kutokea katika historia yetu. Miaka yote minne ya vuguvugu Mwalimu alikaa kimya.  Wafanyakazi wakaitafsiri ukimya wake kama ishara kwamba alikuwa anawaunga mkono. Hawakutarajia kilichofuata. Mei mosi 1974 Mwalimu katika hotuba yake akawakaripia sana wafanyakazi. Aliwalaani kusababisha vurugu. Akasahau alichosema mwenyewe. Mabadiliko makubwa, hususan mapinduzi, vurugu linatokea – vurugu kwa wanyonyaji, aliwahi kusema Mwalimu. Mapinduzi sio lelema

Hotuba ya Mwalimu ya Mei mosi ilivunja moyo wa wafanyakazi. Kilichofuata ni kuwafukuza fukuza wafanyakazi. Walibebewa katika malori; wakachukuliwa vituo vya polisi. Wakachukuliwa alama za vidole kama wahalifu. Wakilindwa na FFU wenye silaha wakahamishwa vijijini vyao. Yaani walalahoi hawana haki ya kuishi mijini. Si kwao. Kwao ni vijijini! Ndio ulikuwa mtazamo wa wakolini. Ndio mtazamo wa watawala wetu! 

Mwalimu kapoteza nafasi adhimu ya kihistoria ya kulikuza tabaka lililoainishwa katika Azimio la Arusha kama msingi wa Ujamaa. Akachagua upande wa warasimu wake, tabaka chipukizi la mabwenyeye wa kirasimu ( bureaucratic bourgeoisie) ambalo baadae lilikuja kupindua Azimio la Arusha. 

Ndivyo ilivyo tokea kwa wakulima pia.’

Niwie radhi Mpendwa Azimio. Nitahitimisha barua yangu hapa. Wajukuu wako hawajazoea kusoma maandiko marefu. Nitaendelea na simulizi yako wiki ijayo. 

Wasalaam

Issa 

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags