12/05/2024
Mpendwa Azimio
Naendelea na mawaidha yako.
‘Nilikusimulia jinsi mpendwa wako, shuja wako, Mwalimu Nyerere, alivyopoza vuguvugu la wafanyakazi na wakulima. Sasa nikueleze “dhambi” nyingine ya mlezi wangu. Situmii neno dhambi kwa mzaha. Ninatambua uzito wake. Machoni mwa wakereketwa wa mrengo wa kushoto, kusababisha uvunjaji au uvurugaji wa chombo cha wavujajasho ni dhambi. Kwa sababu mbalimbali na katika mazingira tofauti Mwalimu alifanya hivyo.
***
Mnamo 1964, jeshi la nchi liliasi. Hatimaye uasi ulizimwa kwa msaada wa makamando wa Uingereza. Ilishukiwa kwamba baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi walihusika. Wengi waliwekwa kizuizini. Vyama huru vya wafanyakazi vika futwa. Haraka haraka sheria ya kuanzisha chama kimoja cha wafanyakazi kilichoitwa NUTA ( National Union of Tanganyika Workers) kilianzishwa. NUTA kiliwekwa chini ya usimamizi wa Serikali. Katibu Mkuu wake aliteuliwa na rais wa nchi, sio kuchaguliwa na wanachama wenyewe. Kwa nyakati tofauti Katibu Mkuu wa NUTA aliwahi kuwa pia Waziri wa Kazi.
Hii ilikuwa mwisho wa vyama huru vya wafanyakazi nchini.
Wakati wa vuguvugu la wafanyakazi mwanzoni mwa miaka ya sabini, wafanyakazi wala hawukutumia NUTA kama chombo chao. Hawakuwa na imani nacho. Badala yake walitumia Kamati za Wafanykazi viwandani. Kamati hizo hazikuwa na uhusiano wowote na NUTA. Pia wafanyakazi walitumia matawi ya TANU.
Baada ya ile hotuba ya Mei mosi ya Mwalimu, sheria ilipitishwa kuzifuta Kamati za Wafanyakazi na kuyaweka rasmi matawi ya NUTA viwandani.
Huu ni mfano mwingine kuonyesha kwamba Mwalimu alizima jitihada zozote za wavujajasho ambazo zilikuwa huru na kutoka chini. Kwa vitendo vyake, Mwalimu alidhihirisha kwamba hakuwa na imani na wafanyakazi na wakulima na uwezo wao wa kutetea haki zao na hatimaye kujikomboa. Alikuwa na imani kubwa na dola yake na warasimu wake, sio wananchi wake.
Ndivyo pia ilivyotokea kwa wakulima. Miaka ya hamsini vyama vya ushirika, kama vyama vya wafanyakazi, vilikuwa na nguvu kubwa sana na walishirikiana na TANU katika mapambano ya uhuru. Baada ya uhuru serikali ilishawishi na mara nyingine baadhi ya viongozi kulazimisha uanzaji wa vyama vya ushirika. Mnamo 1966 iliteuliwa Kamati ya kuchunguza vyama vya ushirika. Kamati iligunduwa rushwa na ubadhirifu katika vyama vingi. Vyama havikuendeshwa kwa njia ya demokrasia. Hata hivyo hakuna la maana lililofanyika kuboresha hali ya vyama hivyo.
Mnamo 1976, kutokana na baadhi ya viongozi wa chama na serikali kulaani sana vyama vya ushirika, vyama vikafutwa. Ni kweli vyama vilikuwa na mapungufu mengi sana. Lakini huutibu ugonjwa kwa kumuua mgonjwa! Hii ilikuwa mwisho wa vyama huru vya ushirika. Baada ya miaka michache Mwalimu alikiri kwamba kuvifuta vyama vya ushirika ilikuwa kosa. Vikarudishwa lakini kama jumuiya ya Chama na chini ya usimamizi na udhibiti wa serikali.
Vyama vya vijana na hasa vyama vya wanafunzi wa Chuo Kikuu pia vilifutwa. Chama kimoja cha wanafunzi wote kilianzishwa chini ya uangalizi wa youth league ya Chama Tawala.
Kwa kifupi, chini ya utawala wa Mwalimu, hakuna organesheni huru iliruhusiwa. Haki ya watu kujikusanya na kuviunda vyombo vyao huru kutetea haki zao haikuwepo kabisa. Jambo hili si dogo. Kuua uwezo, ari na ubunifu wa umma kuunda vyombo vyao bila kuingiliwa ni sawa na kutwaa utu wa binadamu. Vyombo vya umma vina nafasi ya kipekee katika jamii kudhibiti watawala na kuzianika dhambi zao hadharani. Kutokuwa na vyombo huru vya umma inaachia ombwe katika jamii, ombwe ambalo linakuja kujazwa na vyombo vya mabavu na vikundi vya watu wenye sifa maalum ya kujipendekeza na kuimba sifa za watawala kama kasuku.’
Mpendwa Azimio, nimejitahidi kuandika yale uliyoniambia ndotoni. Ninaamini nilikukariri vizuri. Utaniwia radhi kama nimekumezesha maneno au fikra zangu.
Kabla sijamaliza nina ombi maalum. Niruhusu katika barua yangu ijayo tutafakari pamoja na wajukuu wako mafunzo na masomo tunayoyapata kutoka historia yetu na mawaidha yako mazito.
Wasalaam
Issa



Leave a comment