02/05/2024
Issa: Mzee Ngombale tulifanya mahojiano mawili wakati wa uhai wako. Tulizungumzia historia yako binafsi na siasa zako katika CCM. Kwa hivyo, sitayarudio hayo.
Mimi napenda tulizungumzie jambo moja ambalo limekuwa linani tatiza sana. Bahati mbaya nilikosa nafasi ya kulizungumzia hilo wakati wa uhai wako.
Wakati wa mchakato wa kusimamisha mgombea urais 2015, CCM kilipindapinda taratibu zake ili kukwepa kumsimamisha hayati Edward Lowassa. Wewe binafsi ulichukia sana na kukosoa Chama chako. Mimi sina shida na ukosoaji wako isipokuwa ukaenda mbali na kumuunga mkono Lowassa alipokuwa anafanya kampeni kama mgombea urais wa Chadema. Hili sikulielewa kabisa.
Nini ilikufanya udandie safari ya Lowassa kuingia Ikulu? Yaani sifa gani za Lowassa zilikuimpress kiasi cha kumfanyiya kampeni?Wewe, kweli na kwa dhati, ulimuona Lowassa kama mtu safi ambaye anafaa kuwa rais wa nchi yetu wakati ilikuwa inajulikana kabisa kwamba Lowassa alitaka urais kwa gharama zozote zile? Ukweli ni kwamba kilichokuwa kinamsukuma Lowassa kutaka urais kilikuwa personal ambition kuliko maslahi ya nchi ….
[Hata kabla hajamaliza Ngombale kamkatisha Issa.]
Ngombale: Sikiliza Issa. Nyinye vijana wa Chuo Kikuu mlielewa vizuri nadharia ya Kimarx lakini hamkujua hata chembe jinsi ya kufanya siasa. Baada ya kukosoa CCM na kutokuunga mkono chaguo lao la Magufuli, ninge fanya nini? Ulitaka nikunje mikono, nifunge mdomo na kuwa mtazamaji, kweli? Mtu ambaye amekuwa politically active maisha yake yote aende kupumzika sebuluni kwake…!
[Issa kadakia … ]
Issa: Komred je kwako kufanya siasa ilikuwa na maana moja tu – kupanda jukwani na kupigia debe chama cha kisiasa na kiongozi wake bila kujali itikadi ya chama chenyewe au mtazamo wa kiongozi wake? Yaani hukujali maslahi na matakwa ya kitabaka ya wafanyakazi! Hukufikiria kabisa kufanya siasa mbadala?
Ngombale: Ulitaka niingie underground! Hatukuwa na mazingira na vyovyote vile mimi sio muumini wa siasa za akina Lenin ambazo zinafanywa na makada wateule. Mimi ni muumini wa siasa za umma, mass politics.
Issa: Komred wewe ulikuwa Marxisti aliyebobea lakini hapa nadhani umekosea. Lenin aliamini sana katika siasa za umma, lakini siasa za kitabaka. Aliwahi kusema: real politics are where the masses are. Mahala pa siasa halisi ni miongoni mwa umma.
Narudia swali langu. Yaani wazo la siasa mbadala au hata kujitoa kutoka CCM na kuanzisha chama chenye mrengo wa kushoto halikuiijia?
Ngombale: Komred mimi nilikuwa ninaelewa CCM vizuri sana kuliko wewe. Nilikuwa jikoni kabisa. CCM wangeona kujitoa kwangu ni kuvunja CCM na kamwe wasingekubali. Wakereketwa wa CCM wangeniwinda kama kuku.
Issa: Lakini, Mzee, Mwalimu mwenyewe alitamani wakati wa G-55 CCM kungegawanyika (split) na vijana kuanzisha Chama chao cha kijamaa …
Ngombale: Je CCM kiligawanyika? Hakikugawanyika. Kwa nini? Kwa sababu viongozi wanaijua CCM kama kiganja cha mkono wao. Walijua uhai wao kisiasa unategemea chama na machinery yake. Kamwe hawawezi kujiondoa na pia hawawezi kukubali wengine wajiondoe. Atakayejaribu sio tu atawindwa lakini atapakazwa matope na kukashifiwa mpaka asalimu amri. Kwani umesahau? Wangapi walihama vyama vyao vya upinzani na kurudi CCM pamoja na Lowassa mwenyewe!
Komred Issa, nadharia ni kitu kimoja na siasa ni kitu kingine. Kamwe msipuuze siasa za kibwenyeye na mbinu zake.
Issa: Pamoja na kutokupuuza petty bourgeois politics, Komred unatakuniambia tukubali kumezwa na siasa za kibwenyenye!
[Ghafla nikaamka kutoka ndoto zangu za mchana. Nikabaki nikiduwaa. Bado nikabaki na swali: unafanyaje siasa za mrengo wa kushoto kwa mtazamo wa kifanyakazi chini ya himaya ya siasa-tawala za kibwenyenye bila kumezwa? Bila ya kuteketezwa?
***
Fikra-gonganishi juu ya kifo cha Mzee Kingunge Ngombale- Mwiru na masomo yake
Sun, 04 Feb 2018 19:45:45
Issa Shivji
Kifo cha Kamaradi Ngombale kimeamsha msongamano wa fikra, mawazo, tafakuri, zote pamoja, kwa wakati mmoja, kichwani mwangu. Sisemi, wala simaanishi, kwamba nimechanganyikiwa. La hasha! Sijachanganyikiwa. Nachotaka kusema ni kwamba fikra-gonganishi, mawazo matamu na machungu, ya matumaini na ya hofu, yote, kwa pamoja, yawasiliana, yazungumza, yabishana, yatofautiana, yagombana, yaafikiana, kwa wakati mmoja, katika kichwa kimoja, kichwa hichohicho, usiku na mchana. Tangu mzee afariki, nikiamka asubuhi, ninapanga kwenda nyumbani kwake kutoa pole kwa ndugu na marafiki kama ilivyokuwa kawaida yetu. Lakini, kwa sababu za kina, sio za visingizio, ambazo nashindwa kuzibainisha, mpaka leo (Jumapili) sijaenda. Uamuzi wangu wa mwisho sasa ni kwenda kutoa heshima zangu za mwisho Karimjee na kwenda kuuzika mwili wake Kinondoni. Nimetumia maneno “mwili wake” makusudi. Siziki fikra zake (wala zangu) pamoja na yeye. Zile zitaendelea kugongana. Fikra zina maisha yake huru ambazo hazina kikomo na haziendani sambamba na maisha ya mwili ambayo yana kikomo.
Hayo niliyoandika yamekaa kifalsafa-falsafa kidogo. Mzee Ngombale hakuwa mwanafalsafa wala hakuandika kifalsafa. Aliandika kiitikadi na kisiasa. Lakini wanadamu wote hatimaye ni wanafalsafa. Na mwanadamu ambaye aliyewahi kuweka fikra zake, utashi wake, mitazamo yake katika kumbukumbu za kimaandishi au za kidomo, anaamsha, bila kuchokozwa, fikra za kifalsafa.
Nikashindwa kujizuia. Ari ya kuandika hizi fikra-mchanganyiko zangu zimeshinda. Nikaziandika. Fikra zikiandikwa basi sio zako tena. Zina haki za kuwa na maisha yake huru, kwenda popote pale zitakayo, kuruka na kurushwa. Hamna nguvu za kuzizuia hata kwa mabavu. Ni kama mbelewele (pollen) unaoruka kutoka ua mmoja na kurutubisha ua mwingine. Kwa upande wangu, sitaki kuzungumzia wasifu wa Mzee. Hayo yameorodheshwa, na kurudiwarudiwa na wanasiasa wenzake na wanahabari. Anastahili kabisa yote mazuri yaliyosemwa juu yake kuhusu maadili na msimamo wake. Mie sina mengine mapya ya kuongezea. Niwaachie tu wenzi wake wa zamani waendelee kujazia. Kwa upande wangu, ninataka niwashirikishe katika “ugomvi” unaonisumbua, ugomvi wangu wa kifikra kichwani mwangu. Yaani nataka kuwashirikisha nyie katika huo msongamano ninaozungumzia, ambao hautaki kuniacha. Kulikuwa nini yasiyo ya kawaida katika maisha, fikra, vitendo, siasa na itikadi ya Ngombale ambayo ina nguvu isio ya kawaida kuamsha fikra ambazo zinakataa kukaa kwenye maandishi ya kawaida bila msaada wa dhana za kifalsafa? Hili ni swali; sina jibu. Hata hivyo, ninataka kunukuu matukio (episodes) mawili hivi ninayofahamu mie binafsi kuelezea fikra zake ambazo zinagongana. Nitaziita fikra-gonganishi (contradictory ideas).
1
Mnamo miaka ya sabini, sisi vijana wa USARF (University Students African Revolutionary Front) na haswa wa TANU (Tanu Youth League) tulikuwa tunafuatilia kwa karibu siasa za Ngombale. Wachache wetu walikuwa karibu naye, na mtu ambaye alikuwa karibu sana na Ngombale alikuwa hayati Henry Mapolu. Henry alitokea Chuo cha Kivukoni. Ngombale na yeye walikuwa wakufunzi Kivukoni pamoja. Katika miaka hii ya vuguvugu za Azimio la Arusha na Mwongozo wa 1971, Ngombale alijikuta katika mstari wa mbele. Hata hivyo, sisi vijana hatukupendezwa jinsi Mwalimu alikuwa anamtumia, akimhamisha kutoka cheo kimoja kwenda kingine, eneo moja kwenda eneo lingine. Tukahisi anachezewa, anapigwa teke kama mpira. Henry kamandikia barua ya wazi katika jarida letu la MajiMaji. ‘Kwanini Komred unakubali kuchezewa kiasi hicho?’ Hakujibu. Sidhani kwamba walizungumza jambo hilo kifaragha lakini kama walizungumza Henry angetuambia. Hakutuambia. Miongo takriban minne baadai, Henry alipofariki, nikasoma utenzi niliyomtungia. Mzee Ngombale alikuwepo. Nikaja kwenye beti hizi kuhusu ile barua:
Nimemuona rafiki yako wa siku zile za Kivukoni Mzee wetu, mzee Ngombale wa Kiliwani Alikuwa anakuulizia juzijuzi
Nipashe za Kamaradi Henry asiye na upuuzi
Sikuwa na ujasiri wa kumkumbushia
Barua yako ya wazi ulomrushia
Uonjo mkali wa kalamu yako katili
‘Ewe kamaradi wangu wa prolitari
Usikubali kupigwa teke na siasa za jemadari’
Nikamtupia macho Ngombale aliyekuwa amekaa mbali kidogo. Nikamuona ana tabasamu! Tulipomaliza tukakutana. “Nakumbuka”, alisema kwa kicheko. Nikajiuliza. ‘Kicheko hichi kina maana gani?’ Kuna tafsiri mbili. Ama kilikuwa cha dharau: ‘Nyie vijana bado hamja pevuka kisiasa. Hamuwezi kuelewe hizi siasa na wala hamuna stahili au hadhi ya kueleweshwa.’ Au kicheko kilikuwa kinasema kwa unyeyekevu: ‘Ninakubaliana na nyie, mko sahihi, lakini…..’. Hili neno‘lakini’ ndio limebeba jambo zito. Tafsiri moja, kwa maoni yangu, ni kwamba yeyote yule wa mrengo wa kushoto, hususan mwenye itikadi ya U-Marx, hana budi ajue jinsi ya ‘kufanya siasa’ katika mazingira halisi, sio mazingira ya kufikirika. Katika enzi za chama kimoja, chenye siasa na utaifa wa kimaendeleo na nchi yenye kiongozi ambaye anakubalika, ana mwelekeo wa watu kupinga ukoloni na ubeberu na kupigania ukombozi wa Afrika, huwezi, wala sio busara, kupingana naye eti hafuati mwelekeo wa Kimarksi! Hakuna atakuelewa wala kukuunga mkono. Utapotea kutoka rada ya siasa! Kama tafsiri yangu hii ni sahihi basi ina masomo kama matatu muhimu ambayo yanatufundisha jinsi ya kufanya siasa:
Moja, kuwa na unyeyekevu wa kiitikadi badala ya kiburi na majivuno ya usahihi na usafi wa mtazamo wako. Pili, muwe wabunifu katika siasa; kujua unaweza ukafanya nini katika mazingira yapi bila kusaliti mtazamo wako wa kitabaka. Na,
2
tatu, kwa vyovyote vile, kwa mikakati yoyote ile, kamwe kutokusaliti maslahi na matakwa ya tabaka la wavujajasho. Yaani, huwezi ukawa na mikakati ya kisiasa inayoridhia itikadi na nadharia ya kibepari.
Tukio la pili: Katika mkutano mkuu wa nne wa CCM huko Chimwaga, chama kiliridhia kufunguwa milango yake kwa mabepari na wafanyabiashara. Kwa hivyo, CCM, ambacho kilijitambulisha kama chama cha wakulima na wafanyakazi, sasa kikakubali kuwa chama mchanganyiko wa matabaka yenye maslahi yanayogongana. Mzee Ngombale ndio alitoa hotuba yaliyo orodhesha sababu za kufanya hivyo na kuhalalisha tendo hilo, akitumia kwa ufasaha uelewa wake mkubwa wa U-Marx. Mie niliandika makala katika gazeti la Family Mirror nikimdadisi komredi, ‘kulikoni?’ Baada ya miongo kama miwili nilipokuwa na mahojiano naye nyumbani kwake (angalia: Chemchemi 2009) Mzee akakumbuka: “Najua baada ya uchambuzi ule uliandika na kunikosoa na kuniiita mtu hatari sana, lakini sikutaka kukujibu kwa sababu wewe ni rafiki yangu sana.” Napenda kusisitiza maneno haya: ‘rafiki yangu sana’. Alimaanisha nini? Kwa sababu, mie sikuwa rafiki yake kwa maana ya kawaida ya urafiki – kutembeleana, kukunywa bia pamoja (huko “leaders club”!) n.k. Kwa hivyo, urafiki aliyoumaanisha bila shaka ni urafiki wa itiikadi. Na kama ni hivyo, basi hakuona vema kunijibu, kwa maana ya kuingia katika mabishano ya hadhara na rafiki yako wa kiitikadi kwa sababu wote mpo katika mrengo uleule, isipokuwa mnafarakana juu ya mambo fulani fulani. Somo la tukio hili ni jinsi ya kushughulikia mifarakano (migongano) miongoni mwa marafiki wa kiitikadi. Pamoja ni hii, Mzee Ngombale hakunisusia wala hakunichukulia kama ‘adui’ wake, wala hakufikiria kulipiza kisasi. Hili pia inaonyesha sio tu unyeyekevu lakini pia kupevuka kwa siasa, tabia na hulka inayotokana na itikadi na mtazamo wa kivujajasho, hususan Umarksisti.
Ningeweza kuzungumzia matukio mengine ambayo ni ya kisiasa moja kwa moja lakini huu sio muda muafaka wa mjadala huo. Isipokuwa, huko mbele ya safari vijana wenye mtazamo wa kimaendeleo hawana budi wa kujadili fikra za Kamaradi Ngombale katika muktadha wake wa itikadi na mazingira halisi ya nchi yetu wakati ule.
Issa Shivji 4/02/2018
3



Leave a comment