3 Mazungumzo ya kufikirika kati ya TanzaniTuliyonayo (almarufu Tuli) na TanzaniaTuitakayo (almarufu Tata)

9/06/2024

Tuli: Yaani, kijana mwenzangu, bado unazurura mitaani ukitafuta ajira?

Tata: Ndio. Siko peke yangu. Karibu milioni mbili ya kaka na dada zangu na wadogo wangu hawana ajira. Wengine wahitimu wa vyuo vikuu. 

Tuli: Ya mamilioni yanakuhusu nini. Ya kwako inakushinda! 

Tata: Unafikiri nina ngozi ya punda nisihisi tabu za wenzangu!

Nchi gani hii ambayo inashindwa kuwapatia vijana wake ajira? Eti tunahubiriwa siku kucha tujiajiri. Tuwe wajasiria mali. Yaani vijana wafurike mitaani kuchuuza maplastiki ya Wachina! 

Tuli: Wewe Tata una matata mengi. Usiwe mkaidi. Nchi yetu ime noga. Uchumi wake unakua. Nchi za Ughaibuni zinatuheshimu. Sio tu tunakopesheka bali tunakopeshwa matrilioni ya dola. Njo ujiunge na jumuiya yetu, JUMA, jumuiya ya machawa, ufurahie matunda ya mikopo! Mungu akikujalia hata uongozi unaweza kupata. 

Tata: Unamaanisha Mkuu akinijalia!  Hapana. Mimi si kupe niishi kwa kunyonya damu ya binadamu. Na wala sijasomea “taluuma” ya kujipendekeza pendekeza. 

Tuli: Eti ‘usiwe kupe, ujitegemee’. Zile nyimbo za Azimio. Achana nazo. Nenda na wakati. Hatutaki tena kujifungia. Tumefungua milango.  Tunataka kuwa sehemu ya ulimwengu wa sasa. Tunapata wawekezaji. Hata Wazayuni wanapenda nchi yetu. Tunapata mamilioni ya watalii. Mie nimepeleka ombi langu la kuwa tour guide – si nilisomea historia Chuoni! Nasikia kuna waombaji zaidi ya elfu moja. Lakini sijali. Uchawa wangu utanisogeza. Nina uhakika. Unaona faida ya uchawa?

Tata: Duh! Hata aibu huna. Yaani unajinadi kama chawa! Hapana. Nchi gani hii!

Mimi nataka vijana wenzangu wawe jeuri. Wadadisi kila kitu. Wawe tayari kujenga nchi itakayojitegemea; nchi yenye usawa na utu; nchi inayojali maendelea ya waliowengi; nchi inayolinda uhuru wake na uhuru wa kila mwananchi; nchi inayoamini wataalam na vijana wake; nchi inayo Dira na Maono unaoweka utu mbele … naam ndio Tanzania ninayotamani. 

Tanzania ninayotamani itajitosheleza kwa chakula. Hatutakuwa omba omba. Tanzania inayosindika mazao yake yenyewe. Sio kusafirisha nje kama malighafi. Tanzania inayo chakata madini yake ili kunufaisha wananchi wake. 

Tuli: Wewe baki na ndoto zako za Abunuwasi. Mimi naenda zangu. Niwapigie simu wanaohusika waniweke mbele katika usaili wa kesho. 

*** ***

[Baada ya wiki moja Tuli na Tata wanakutana tena mitaani]

Tata: Je rafiki yangu bila shaka umepata kazi? Kampuni yako inaitwa je?

Tuli: (kwa sauti ya unyonge). Hapana. Nilpoenda usailini nikakuta hakuna jina langu katika short list ya watu ishirini. Niliona majina mengi ya ndugu za viongozi. Nchi hii! Na isitoshe wenzangu wa JUMA wakakataa kunipokea, eti wanasema niliwatumia, nikapanda mabegani yao, kujipendekeza kupata ajira. Nchi hii! Kweli ndio Tanzania tuliyonayo, kweli … ? ( akaanza kububukiwa na machozi)

Tata: Tulia rafiki yangu. Usilie. Achana na uchawa. Achana kujipendekeza kwa wachumia tumbo. Ujiunge nasi tujenge Tanzania mpya. Tanzania yenye haki; nchi inayojali watu wake bila kujali nyadhifa zao, nchi ambamo kila moja ana haki na heshima bila kujali hali yake.

Safari ni ndefu lakini kila safari ina mwanzo. Sisi – wewe, mimi na mamilioni wa vijana wenzetu – tuwe waanzilishi wa safari hii ya ukombozi wa pili. Tuwe waasisi wa vuguvugu la Tanzania mpya. Historia itatukumbuka. 

[ Tuli kasimama kutoka jiweni alikokaa. Akamkumbatia Tata. Akashika mkono wake. Tata katoa kofia kutoka mfukoni mwake. Akamvisha Tuli. Wakatabasamu. Wakaanza kutembea… bega kwa bega, hatua kwa hatua …. . Naam kila safari ina mwanzo. Wakasimuliana hadithi za kale. Hadithi za bibi.]

Tuli: Matata unakumbuka ile hadothi ya mama jongoo na mtoto jongoo. 

Tata: Nimewahi kuisikia lakini sikumbuki vizuri. 

Tuli: Mtoto jongoo amamuuliza mama yake. Mama, mama nitangulize mguu gani?  Mama jongoo anamjibu:  tembea mwanangu, tembea. 

***

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags