23/06/2024
Issa: ni karibu muongo mmoja na nusu tangu utuage. Mzee Duncan wewe ulikuwa kati ya wanachama waanzilishi wa HAKIARDHI. Ulisaidia sana kuuimarisha msimamo na ukereketwa wa vijana wa Hakiardhi. Pamoja na changamoto lukuki wameendelea kuweka hai Taasisi tuliyojaribu kujenga pamoja. Ili kuwakumbushia wana wa Hakiardhi aina wa mtu ulikuwa ninashare nao utenzi nilioutunga na kusomwa wakati wa mazishi yako.
***
Buriani Mzee Duncan
Kwa Nini?
Mzee wangu, Mzee Duncan.
Miye siyo mtunzi mashuhuri, wa shairi.
Miye siyo mwandishi mahiri, wa riwaya.
Kwa kuomboleza kifo cha mzee wangu,
Sihitaji kuwa msanii.
Moyo wangu unadunda, unaimba.
Sauti anapepesuka,
Shairi anasusiya,
Riwaya anasononeka,
Wimbo anagomba.
Wasanii wamekuja juu,
Wote kwa sauti wananikaripia:
“Wee fidhuli wee,
Usitufedheheshe,
Usituaibishe.
Eti, unajifanya mtoto wa Mariam,
Kana kwamba unamiliki jina-Issa.
Potelea mbali,
Wasanii na usanii wao.
Leo nitaimba!
Nitajigamba, mimi Issa bin Mariam.
Nitaimba kuomboleza kifo cha Mzee wangu,
Mzee Duncan Getakanoda.
Miongo mitatu iliyopita,
Tulionana, ukiwa kada wa chama,
Huko kigamboni,
Chuo cha Kivukoni,
Kitovu cha itikadi,
Itikadi ya ujamaa.
Itikadi ukaisoma.
Ukaipapasa kwa undani,
Ukaipindua juu chini,
Ukaibua lukuki ya maswali,
Maswali yasiyo na majibu.
Kwa nini watu wangu, Wadatoga,
(Eti huitwa Wabarabaig!)
Kwa nini, hutekwa ardhi yao?
Kwa nini, hufa na mifugo yao?
Kwa nini, utu wao hudhalalishwa?
Mashamba yao hutaifishwa,
Mashamba yao hubinafsishwa.
Haki zao huponyokwa.
Kwa nini?
Kwa nini, binamu zangu Wamaasai,
Hukosa elimu, afya na maji?
Kwa nini wajomba zangu Wanyaturu,
Hubaguliwa, huadhibiwa kijumla?
Kwa nini?
Ukatembea na miguu,
Ukapanda mabasi,
Ukakodisha magari,
Ukaenda Dodoma.
Ukaonana na viongozi wa chama,
Heshima zao hazikutetemesha.
“Kwa heshima na taadhima,
Nawaulizeni, siwadadisi, nawauliza tu:
Kwa nini watu wangu huteswa?”
Ukapanda mabasi, na matreni,
Ukafika bandari ya salama.
Ukamwuliza Waziri Mkuu,
Ukuu wake haukukutisha.
Ukamuliza: Kwa nini?
Ukawalilia mawakili,
Mashauri ukayafungua,
Ushupavu ukauonyesha.
“Mashamba yetu ya ngano,
Mheshimiwa Jaji,
Yamefukiwa na buldoza,
Makazi yetu yamechomwa,
Jamii zetu zimesambaratishwa.
Je, hii ni haki?
Kwa nini?
Ushindi wa kimahakama,
Ukawa kilemba cha ukoka.
Ukakamatwa na polisi,
Ukawekwa ndani,
Ukafunguliwa mashtaka,
Eti, umediriki kudai haki za watu wako!
Mwanafunzi makini,
Mzee Ducan kajifunza,
Somo la awali:
“Naam. Wakubwa ni wakubwa!
Maslahi yao siyo yangu,
Maslahi yangu siyo yao.”
Akajiunga na HAKIARDHI,
Umoja ni nguvu, chombo ni muungano.
Mnyonge hana kabila,
Hana rika,
Hana jinsia,
Ana unyonge tu.
Hukuchoka, hukukata tamaa.
Vijana ukawashawishi,
Wazee ukawaunganisha.
Mapambano siyo lelemama,
Umoja wetu, ndiyo mkuki wetu.
Chombo chetu, ndiyo ngao letu.
Buriani mzee wangu,
Mzee Duncan Getakanoda.
Kwa moyo mzito,
Anakuaga Issa bin Mariam.
Nenda salama, upumzike mahali pema.
Somo lako tutalifundisha,
Kamwe hatutalisahau.
Mapambano ni marefu,
Undani wake mjielewe,
Upana wake mjitambue.
Kamwe msisalimu amri,
Mbele ya ukatili, ukandamizaji na dhuluma.
Dhuluma ni adui,
Adui wa Wana wa Adamu.
Issa bin Mariam
Juni 03, 2008
***
Hii ni makala ya mwisho katika mfululizo wa Mazungumzo ya Kufikirika. Kuanzia wiku ijayo nitaanza mfulilizo wa makala ‘Tulipo, Tunakoelekea’



Leave a comment