’tulipo. Tunakoelekea.’ 3 Tafakuri ya kila wiki. Ukuaji wa uchumi bila ukuaji wa ajira. (Jobless growth)

14/07/2024

Kwa miaka michache sasa takwimu rasmi za serikali zinaonyesha ukuaji wa uchumi kwa asilimia kati ya 4 na 5. Kwa mwaka wa 2024 inatarijiwa ukuaji wa uchumi utaluwa kama asilimia 5.6. 

Ukuaji uchumi peke yake sio lazima dalili ya maendeleo au dalili ya uboreshaji wa maisha ya wananchi. Takwimu moja wapo ya kuangalia kila mara tunapoongea ukuaji kuangalia takwimu za ajira. Na katika hili Tanzania kama nchi nyingi chini ya mfumo wa uliberali mamboleo hali ya ajira sio kutia moyo. Hatuna budi tuangalie takwimu chache zihusuyo  ajira na shughuli za kiuchumi za wananchi kwa jumla. 

Tanzania ilikadiriwa kuwa na watu milioni 58.4 mwaka wa 2020. (Ninachukua mwaka huu kwa sababu takwimu zilizokusanywa kuhusu ajira ilikuwa katika mwaka 2020.) Kati ya hao milioni 32 ni wenye umri wa kufanya kazi. Kati ya hao milioni 27 wako katika shughuli za kiuchumi na takriban milioni 5 hawahusiki na uchumi kabisa ( k.m wastaafu, wsiojiweza, wazee n.k.). 

Takriban watu milioni 24 wana ajira, wengi wao (asilimia 61) wakiwa katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi wakifuatiwa na asilimia 29 katika sekta isiyorasmi na asilimia 10 tu katika sekta rasmi. Sote tunafahamu kuwa walioko katika sekta isiyorasmi hua wanaishi maisha magumu sana. Ujira wao ni mdogo, hawana siku za mapumziko wala likizo wala manufaa mengine kama bima la afya. Watoto wao wana kosa elimu. Inawabidi wao pia wafanye kazi kumudu mahitaji ya lazima. Wote, baba, mama na watoto wafanye kazi masaa marefu ili kuishi tu. Ajira zao hazina uhakika. Ni vibarua wasiona matumaini ya kesho. Kwa hivyo, kuwa na takriban thuluthi moja ya watu katika sekta isiyorasmi sio jambo la kulijivunia bali ni dalili ya ugonjwa wa uchumi wetu. 

Asilimia 10 tu kuwa katika ajira rasmi ni dalili ya uchumi kombo. Na tarakimu hii haija badiliki sana katika miaka mitano hivi pamoja na ongezeko katika uwekezaji kutoka nje na mikopo lukuki. 

Niongeze tarakimu nyingine ambayo pia ni muhimu ya kusisitiza. Kama asimilia 40, yaani watu wanne katika kumi, wako katika ajira inayoitwa precarious kwa maana ya ajira iliyona mashaka na wasiwasi. Hao wanakosa uhakika wa kazi. Tunaweza tukasema kwamba kundi hili lina angukia kati ya watu katika sekta isiyorasmi na sekta iliyorasmi. 

****

Sasa tarakimu muhimu sana na kutilia maanani ni ile ya watu wasiona kazi (unemployed). Wasiona kazi ni takriban milioni 2.5, milioni mbili na nusu. Walio wengi katika kundi hili ni vijana kati ya umri 15-24 na 25-35. Vijana wengi wasiona kazi ni wahitimu wa shule za msingi na sekondari (asimilia 14) lakini asilimia wasiona kazi inapungua sana katika kundi ambalo halijaenda shuleni kabisa. Vijana wenye elimu wasiona kazi ndio Gen-Z na walikuwa chachu ya maandamano katika nchi jirani ya Kenya. 

Hata wataalam wenye shahada za Vyuo Vikuu wameathirika; wanakosa ajira. Juzijuzi kulikuwa na taarifa katika gazeti la Mwananchi kwamba madaktari 5000 na manesi 25000 hawana ajira ( Mwananchi 8/07/2024). Hii ni wakati zahanati na mahospitali zetu zina uhaba wa madaktari. Serikali inadai haina hela ya kuwaajiri. Je kweli serikali haina hela? Vipi serikali hiyo hiyo intenga mabilioni kununua magari ya kianasa kwa ajili ya watendaji na viongozi wa ngazi za juu? Waziri wa Fedha katika hotuba yake ya bajeti alisema serikali hutumia sh bilioni 558.4 kila mwaka kununua magari, vipuri na gharama za kununua mafuta na kwa ajili ya matengenezo. 

Mhitimu wa udakatari hupata mshahara kati ya laki nne na laki tisa. Tukichukuwa mshahara wa milioni moja na kupiga hesabu tunakuta sh bilioni 558.4 inatosha kuajiri madakatari takriban 465,000 kila mwaka. (1,000,000 x 12 = 12,000,000.  558,400,000,000/12,000,000 = 465,333.). Kwa maneno mengine ukipunguza tu bilioni 6 katika bajeti ya magari unaweza ukaajiri madaktari 5000 kwa mwaka. 

Hitimisho

Pamoja na ukuaji uchumi, uwekezaji, ujenzi wa miradi mbalimbali n.k. bado idadi ya watu wasiona ajira ama inaongezeka au inabaki pale pale. Inakadiriwa kila mwaka idadi ya vijana wanaoingia soko la ajira ni 800,000 (laki nane) lakini ajira mpya zinazozalishwa kila mwaka ni 40,000 tu. Kwa takwimu hizi takriban 750,000 wanakosa ajira. Hao ndio wanaoingia katika sekta isiyorasmi au kutafuta hela kwa njia ambazo sio tu sio halali lakini hata ni chafu. Uhalifu unaongezeka, wizi unakithiri, usalama unapotea. Wimbo la maendeleo linakuwa halina maana. 

Ukuaji wa uchumi yenyewe sio ishara ya maendeleo kama wananchi walio wengi wanakosa ajira na wanalazimika kufanya kazi zisizona staha. 

Swali ni: kwa nini tunakuwa katika hali hii? Chanzo chake nini? Tutafakari. Nitachokoza mada hiyo katika tafakuri ijayo. 

*** *** ***

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags