21/07/2024
Uchumi wa uliberali mambo leo unakita kwenye sifa mbili muhimu – moja ni uzalishaji wa malighafi na pili ni kupanua wigo wa biashara ya nje ili kujiingiza zaidi na zaidi katika mzunguko wa bidhaa kimataifa. Kwa kiasi fulani sifa hizi zinafanana na sifa za uchumi wa kikoloni lakini kuna tofauti muhimu. Tafauti ya kwanza ni malighafi tuliyokuwa tunazalisha nyakati za ukoloni yalikuwa mazao ya kilimo – kahawa, chai, pamba, mkonge, korosho n.k. Lakini katika mfumo wa uliberali mamboleo malighafi muhimu tunayozalisha ni madini – dhahabu, almasi, gesi asilia, na rasilimali zingine zinazopatikana katika misitu yetu kama mbao na bioresources pamoja na plazma ya mbegu (seed plasma).
Wataalam wa nje wanachukua plazma za mbegu zetu na kwenda kuzalisha mbegu (wao wenyewe wanaiita mbegu bora yenye tija) katika maabara zao wakichanganya na kemikali zingine na kufanya ukarabati katika jenetiki (genes) zake. Hizi tunaziita mbegu za GMO (genetically modified organism). Kwa maneno mengine “nasaba” ya mbegu inachakachuliwa kuzaa mbegu zenye sifa tofauti na sifa zake za kiasilia. Mbegu hizi huwezi kuzitumia kila msimu. Zinakufa baada ya kutumia mara moja. Zinaitwa terminal seeds. Na mbegu hizi zinaletewa kwetu na tunawauzia wakulima wetu kwa kisingizio cha mbegu bora wenye tija. Hatimaye wakulima wetu wanakuwa wategemezi, wakitegemea mbegu zilizochakachuliwa. Kwa sababu kila msimu wanalazimika kurudi kwenye makampuni ya mbegu kununua mbegu. Hawawezi kuhifadhi mbegu msimu hadi msimu kama walivyozoea kufanya.
Licha ya utegemezi, tafiti zinaonyesha mbegu za GMO ni hatari kwa afya ya binadamu. Nyakati za hayati Rais Magufuli mbegu za GMO pamoja na vyakula vyote vya GMO vilipigwa marufuku. Siku hizi nasikia masharti yamelegezwa. Inawezekana tunalishwa vyakula vya GMO na kuuziwa mbegu za GMO. Tujihadharishe! Uholela wetu usitufanye tufumbie macho kinachoweza kutokea kutakona na matumuzi ya vyakula na mbegu za GMO.
***
Chini ya mfumo wa uliberali mambo leo, pili ni kupanua wigo wa biashara na kutunasa katika mtego wa biashara unaofuata mantiki ya kibepari. Tunashawishiwa kubidhaaisha na kubinafsisha rasilimali zetu pamoja na ardhi, misitu, maji, mito, milima na wanyamapori kwa visingizio mbalimbali – kuongeza tija, kupata fedha za kigeni na kusasaisha uchumi wetu.
Sifa nyingine ya uliberali mamboleo, ambayo haikuwepo wakati wa ukoloni, ni kufedhaaisha (financialise) uchumi. Hii inazaa soko la fedha na sarafu mbalimbali. Fedha yenyewe inakuwa bidhaa ya kuuza na kununua. Tunashinikizwa kuwa na soko huria katika fedha na sarafu yetu. Hatimaye tunanaswa katika mtandao wa biashara ya kifedha. Ikitokea zama za kifedha (financial crisis) basi tunaathirika. Tunashindwa kuhimili zama za kiuchumi. Inatubidii tuwaendee maShylocks, yaani taasisi za kifedha za kimataifa, kuja kutukomboa. Na wao wanakuja na msharti yao magumu ya kutukopesha kama ya kuteka rehani rasilimali zetu na uthibiti wa sekta yetu ya fedha. Kwa kifupi, zama kama hizi ndio inatoa mwanya kwa nchi babe za kibeberu kujipenyeza katika nchi zetu na kuchukua mikononi mwao hatma ya taifa letu. Tunapoteza mamlaka ya nchi (sovereignty) na uhuru wa mwananchi.
Jambo hili sio la kubuniwa bali limewahi kutokea katika nchi mbalimbali kama Sri Lanka na Msumbiji.
Ndipo tulipo. Je tunaelekea wapi? Sioni dalili zozote za kujinusuru kutoka mfumo huo wa uliberali mambo leo. Badala yake naona tunazama zaidi na zaidi katika mfumo ambao nina wasiwasi utatumeza na kutuacha hoi. Siombi itokee hivyo. Lakini maombi hayatoshi. Uhalisia unahitaji uchambuzi wa kina wa hali yetu na hali ya dunia. Unahitaji kwa pamoja kuyajadili hali halisi bila uoga, hofu na kutishana. Unahitaji ujasiri wa kukiri ukweli na kutafuta utatuzi unaotokana na uelewa mpana na wa kina. Uropokaji hautoshi. Sloganeering inatupotosha. Tuachane kulaumiana na kukusoana bila kikomo. Tujifunze kufikirishana, kuhojiana na kudadisiana. Na hakuna yeyote juu ya hiyo. Kila mtu anaweza kudadisi na kila mtu anaweza kudadisiwa.
*** *** ***



Leave a comment