04/08/2024
Kwa Mhe wa Africa tuliyonayo
Bomoa bomoa, bomoa makazi ya wanyonge.
Tumia tumia, tumia dhana ya eti utawala wa sheria.
Pora, Pora, pora ardhi ya walalahoi.
Kwani nani wa kusema sheria zilizopo haitendi haki?
Usijali, usiwe na unyonge
Shikilia kamba ya maendeleo.
Nani mwenye ujasiri wa kuuliza
Maendeleo ya nani?
Tenda kwanza
Halalisha baadai.
Una wabobebezi lukuki
Watatafuta msamiati halilishi wa kisheria.
Nani mwenye ubabe wa kuwapinga?
Ujiridhishe tu unawafanyiya mema wananchi wako
Upate wema duniani na aherani.
Nani ya kujua au kujali
Kitakachotokea mbele ya safari?
Wasalaam
Niko nawe daima
Mwanasiasa chupukizi.
***
Kutoka Kiongozi wa Afrika Tutamaniyo
Ondoeni picha zangu majumbani mwenu
Bomoeni sanamu zangu mitaani wenu.
Kwani mimi ni Mungu wa kuabudu?
Au Mrungu wa kubembelezwa?
Futeni jina langu vituoni
Wekeni majina ya mashujaa wetu
Akina Kinjikitile na Mirambo
Mzee Tambaza na Bibi Titi
Njoni tukaae pamoja
Muunganeni tupange pamoja
Kupambana na ubeberu wa Ulaya
Na ubabe wa Marekani.
Karibuni tufichue vibaraka wao
Watawala vikaragosi.
Madalali wa rasilimali zetu
Wavurugaji wa urathi wetu.
Wasalaam
Mtumishi wenu daima



Leave a comment