18/08/2024
Uchumi wa kibepari unakita kwenye ukuaji (growth). Kipimo cha ukuaji ni ukuaji wa Pato la Nchi (Gross National Product GNP). GNP pia ni kipimo cha ukwasi (wealth) au utajiri wa nchi. Kwa kuwa ukuaji wa GNP unatumika sana kama dalili la maendeleo, ni muhimu kuelewa jinsi GNP linapimwa. Itaeleweka vizuri niki toa mfano. Tanzania ina maeneo makubwa ya misitu. Wenyeji wanatumia misitu kwa manufaa yao: kuni ya kupikia chakula, kuvuna mimea mingine kutengeneza dawa za kinyeji, n.k. Misitu hii sio ukwasi, utajiri, wa nchi kwa sababu haiingia katika kuhesabu GNP. Wala matumizi ya mazao yanayotumika na wenyeji kujistawisha pia haihesabiwi kama ukwasi kwa sababu haingia kwenye hisabu za GNP.
Lakini ukimleta mwekezaji na kumpa eneo la msitu na akianza kukata miti na kusafirisha nje, hii inaingia kwenye Pato la Nchi, inaongeza ukuaji. Tunaisherehekea hata kama wenyeji wanakosa mahali pa kupata mimea ya dawa na kuni ya kupikia. Unaweza kutoa mifano mingi lakini hii moja inatosha. Ni wazi pia kwamba wakati uwekezaji nilioutaja unachangia kwenye ukuaji wa uchumi, udhooifishaji wa ustawi wa wenyeji hauonyeshi kwenye GNP. Sio jambo la kujali.
Sasa hii ndio tunaita maendeleo. Ukuaji wa uchumi (growth) ni maendeleo. Miradi mingi ya maendeleo ni ya aina hii. Mimi ninayaita mandeleo ya miradi nikitofautisha na miradi ya maendeleo ambazo zinaongeza ustawi wa jamii.
Itatusaidia kuelewa dhana ya maendeleo vizuri tukitofautisha kati ya ukuaji wa uchumi ( economic growth) na ukuaji au manedeleo ya jamii ( social development). Ukuaji wa uchumi haunamaana ya kuongeza ustawi wa jamii. Unaweza ukawana ukuaji wa uchumi bila kupunguza umaskini au kuongeza ustawi wa jamii.
Ndio, ukuaji unaongeza mapato ya serikali. Lakini asilimia kubwa ya mapato inakwenda kulipia madeni ya nchi na asilimia kubwa inayobaki inatumika kubeba marupurupu ya watawala wa ngazi ya juu.
Kuna jambo linigine pia hatunabudi kulielewa. Uzoefu wetu unaonyesha kwamba uchumi unaweza ukawa kwa asilimia 5 au 6 lakini huo hauongezi ajira. Yaani uhaba wa ajira unaenda sambamba na ukuaji wa uchumi (jobless growth). Ndio maana tunakuta mwaka hadi mwaka ingawa ukuaji unakuwa, idadi kubwa ya vijana wa rika zote, hasa wale kati ya umri wa 15-24, yaani Gen-Z, inaongezeka.
Na hii ni bomu inayosubiri kulipuka.
Tutafakari. Tusisherehekee au kulenga kwenye ukuaji bila kuyaangalia maendeleo ya wananchi waliowengi. Ukuaji peke yake sio kipimo sahihi cha mendeleo. Maendeleo ni zaidi ya ukuaji. *Development and growth are not the same thing. You can have growth without development.*



Leave a comment