2 barua ya kila wiki kwa mpenzi wangu azimio

18/02/2024

Mpenzi Azimio

Ninajua hukukasirika na barua yangu ya 11/02. Uliponiijia ndotoni ulikuwa unatabasamu. Wala hukusubiri tujuliane hali. Ukanibusu hapa na pale na kila mahali. Ilikuwa raha tupu. Mengine sitaisema. Isije nikaaibika mbele ya hadhira mchana kweupe!

Swali langu linaendelea kunitatanisha. Mlezi wako, Mwalimu wangu mpendwa, kweli alikuumpa hadhi ya kidini? Ninajua Mwalimu alikuwa mtu wa dini. Alipenda sana dini yake. Ingawa pale ilipohitaji hakusita kukosoa taasisi za dini. Hata hivyo siamini alikuona kwa jicho la kidini. Nimesoma na nimerudiarudia kusoma sifa zako zilizoorodheshwa katika kitambulisho chako kinachoitwa Azimio la Arusha. Sikuona popote kuna hata neno la kidini dini. Sifa zako zote, zote asilimia mia moja, ni za kisiasa. Tena sio siasa nyepesi za hao wanasiasa wa vizazi vya leo bali siasa yenye maana, siasa yenye mwelekeo na mtazamo thabiti. Natamani kusema mtazamo wa kitabaka. Lakini sitaki nikuudhi – najua mlezi wako hakuamini katika mambo ya kitabaka. Yeye aliegemea zaidi kwenye mtazamo wa kitaifa na sio kitabaka. 

Pamoja na imani zake nilizozitaja, ukweli unabaki pale pale. Hakuna hata nukta ya dini katika sifa zako zilizoorodheshwa katika kitambulisho chako. 

Baada ya kubungabongo kwa siku kadha nadhani nimepata jibu. Jambo moja lililonisaidia ni kwamba matamko haya ya kukufananisha na Bibilia yalianza kutokeza baada ya Mwalimu kung’atuka madaraka na baada ya kifo chako. Ninakumbuka pia aliwahi kutamka kwamba Azimio litafufuka na Watanzania watarejea kwenye maadili na misingi ya Azimio la Arusha. Mara nyingine tena katumia msamiati wa kidini – kufufuka. 

Sasa wakati  wa uhai wako hakutumia kabisa dhana hizo za kidini. Badala yake alikuwa anakulinda kama  mtoto wa siasia na alikuwa anafananua sifa zako kwa lugha na mantiki ya kisiasa. Ikatokea nini akabadili mwelekeo wake huo baada ya kuacha madaraka ya kisiasa na ya kichama? (Kwa kuwa hukwepo, nikutaarifu kwamba Mwalimu aliachia uenyekiti wa Chama 1989 kabla ya kipindi chake cha uenyekiti kuisha.)

Sitaki nikubore zaidi mpenzi wangu. Katika barua yangu ijao nitajitahidi kujibu swali hili. 

Wakati ukisubiri barua yangu, pokea mahaba yangu yasiyona kikomo. 

Pamoja na mabusu motomoto

Wako 

Issa

3 responses to “2 barua ya kila wiki kwa mpenzi wangu azimio”

  1. Maiko Mwageni Avatar
    Maiko Mwageni

    Asante saana, maarifa safi prof kwa vijana wa leo

    Like

  2. Elimu iliyotukuka na maarifa makubwa ya uwasilishaji. Hongera sana Prof. Shivji.

    Kweli Sheria ni Historia; nathibitisha Kauli Mbiu adhimu ya Mkuu wa Skuli ya Sheria Zanzibar (Law School of Zanzibar), Dr. Ally Uki.

    Like

  3. Bahati Kamando Avatar
    Bahati Kamando

    Kuna haja ya Vijana wa Sasa kupigwa msasa kujua mambo muhimu kuhusu Azimio la Arusha….

    Lakini cha kusikitisha Taifa limedumbukia kwenye mlengo wa hovyo usiotaka Vijana kuhoji na kufikili, Taifa limehodhiwa na kikundi cha Watu na kufanya maamuzi kwa mlengo wa maslahi yao binafsi…. Ni hatari

    Like

Leave a reply to qwyckg Cancel reply

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags