4 BARUA YA WIKI KWA MPENDWA WANGU AZIMIO

3/03/2024

Mpendwa Azimio

Baadhi ya vijana wa kizazi kilichopo watakuwa wamesikia, ama kusimuliwa au kusoma kwamba kipindi cha mwisho (1980-1985) cha utawala wa Mwalimu Nyerere kili kuwa kigumu sana. Bidhaa zilikuwa adimu. Mahitaji ya kawaida kama colgate au sabuni au madawa yalikuwa haipatikani. Kulikuwa na mgao wa vyakula kama unga, mchele, mafuta ya kupikia, sukari n.k. Ilibidi watu wajipange foleni mbele ya maduka ya kaaya na kadi zao ya mgao ili kupata kilo mbili au tatu kwa kutegemea ukubwa wa familia. Viwanda vyetu vikaanza kufanya kazi chini ya uwezo wake kwa sababu hatukuwa na fedha za kigeni kununua vipuri na malighafi. Rushwa iliongezeka mara dufu. Maadili ya watumishi wa serikali na watawala yaliyeyuka. 

Matapeli, wafanyabiashara wenye uchu wa kujitajirisha haraka haraka, madalali na makuadi walitumia uhaba wa bidhaa kama nafasi ya kujichumia mali na kujitajirisha bila haya. Huduma za kijamii zilipigwa bei. Pasipoti ziliuzwa mitaani. Jambo kama hili hutokea katika hali ya vita au zama za kiuchumi kote duniani. Kila jamii ina wabaya wake ambao huona dhiki ya wenzao ni fursa kwao kujitajirisha. 

Bila shaka wasimulizi waliongeza propaganda zao hususan kulaumu ujamaa na ukaidi wa Mwalimu kutokulegeza kamba msimamo wake wa kijamaa. Ndani ya nchi propaganda ya aina hii zilianza chini chini. Nje ya nchi na wanadiplomasia kutoka nchi za kibeberu walikuwa wanaeneza propaganda dhidi ya ujamaa kupitia vyombo vyao vya mawasiliano. Baadhi ya vijana na viongozi wetu walimeza propaganda kama hizi na wakaanza kukashifu ujamaa. Katika mapambano kati ya ubepari na ujamaa ambayo mwisho wa siku ni mapambano ya kitabaka, upotoshaji wa habari na taarifa na kukuza uongo na uvumi ni silaha moja wapo muhimu kushinda vita. 

Ni kweli kwamba hali ya maisha ilikuwa mbaya mno isipokuwa sio sahihi kwamba hali hiyo ilitokana na sera za kijamaa. Nchi nyingi za Afrika bila kujali sera zao za mkono wa kushoto au kulia waliathirika sawia. 

Sitaingia kwa undani sababu za zama za kiuchumi isipokuwa kutaja mambo mawili au matatu yaliyoathiri sana uchumi wa nchi yetu. Moja, nafikiri tulishindwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta yetu ya kilimo. Zana za kufanyiya kazi zilibaki zile zile, jembe na panga. Utegemezi wa mvua wa msimu uliendelea. Tulishindwa kupanua kilimo cha umwagiliaji maji. Pili tuliendelea kulima mazao ya kibiashara kuuza nje badala ya kutoa kipaumbele mazao ya chakula kujitosheleza kwa chakula na kukuza soko la ndani. Tuliendelea kutegemea masoko ya kimataifa yaliyokuwa yanatupangia bei. 

Pili, kama nchi zingine za Afrika, mwanzoni mwa 1970 tulikopa sana bila kuzingatia mahitaji yetu hasa mkakati wa kujenga uchumi wa kitaifa ambamo sekta zinafungamana na kutegemeana. Tulishawishika na kushawishiwa kukopa kwa sababu mikopo ilikuwa inapatikana kwa riba ndogo. Hii ilitokana na soko la fedha duniani kufurika na petro-dollars. Kwa kuwa bei ya mafuta ilipanda sana, mashirika ya kimataifa na mabenki walikuwa na fedha za ziada kukopesha. Mwishoni mwa 70 mikopo ikaanza kukomaa na wakopeshaji kudai walipwe bila huruma. Ilitubidii tukimbilie kwenye taasisi za fedha kama IMF (International Minetary Fund) watukopeshe zaidi ili kukidhi mahitaji yetu ya fedha za kigeni. 

Isitoshe ilitubidi tupigane vita na nduli Idi Amin kwa sababu huyu alivamia nchi yetu. Vita vilitugharimu sana na kuathiri uchumi wetu kwa kiwango kikubwa. Inakisiwa vita vilitigharimu kiasi cha dola milioni 500 ya Marekani. 

Pamoja na kwamba Mwalimu alitangaza hadharani kutokugombea urais 1985, hali ngumu ya uchumi na minong’ono katika chama chake dhidi yake nafikiri iliimarisha zaidi uamuzi wake wa kung’atuka ili mrithi wake aweze kufanikisha majadiliano na taasisi za fedha za kimataifa. Kwa upande wake, fikra zake zilikuwa kurudi chamani kujenga upya nguvu zake za kuendelea kusimamia mtazamo wa kijamaa. Ndivyo alivyofanya. Mara baada ya kuachana na usukani wa dola, akaanza kufanya ziara mikoani kukagua matawi ya chama. Je kule alikuta nini? Je dhamira yake ya kukiongezea chama nguvu ilikuwa na mashiko? Nitayazungumzia hayo katika barua yangu ijayo. 

Wasalaam

Issa

5 responses to “4 BARUA YA WIKI KWA MPENDWA WANGU AZIMIO”

  1. GEOFREY EMMANUELY MSYALIHA Avatar
    GEOFREY EMMANUELY MSYALIHA

    Professor, Mwalimu Nyerere alipong’atuka alianza kuzunguka nchi nzima kukomaza sera ya kijamaa ndani ya chama cha mapinduzi na serikali, na hisitoria inaonesha mwalimu alibaki na heshima kubwa ndani ya chama na serikali. Je, Mwalimu Nyerere alipong’atuka aliendelea kukitumikia chama akiwa na nafasi au cheo gani?

    Like

    1. Kipindi cha Mwalimu cha uenyekiti wa Chama kilikuwa bado hakijaisha. Kiliisha 1987. Nitaeleza katika barua zijazo kuhusu mtazamo wa Mwalimu juu ya uhusiano kati ya uenyekiti wa chama na urais

      Liked by 1 person

  2. Maiko Mwageni Avatar
    Maiko Mwageni

    Asante sana professor kwa maarifa safi

    Like

  3. Asante sana ndugu ISSA SHIVJI naomba ujibu swali la ndugu Geofrey Mwal aliendelea kuitumikia nchi na chama akiwa na cheo gani ???

    Like

  4. jeminfrance98 Avatar
    jeminfrance98

    Ahsante kwa maarifa Prof

    Like

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags