5 BARUA YA Wiki kwa mpendwa wangu azimio

10/03/2024

Mpendwa Azimio

Mwalimu Nyerere aling’atuka madaraka ya Serikali 1985. Mzee Ali Hassan Mwinyi kawa rais. Hii ndio awamu ya pili. Hata hivyo Mwalimu aliendelea na uenyekiti wake wa Chama. Kipindi chake cha uenyekiti kilikuwa kinaishia 1987. 

Kwa fikra zake Mwalimu alitaka asiondoke ghafla. Ajaribu kuisaidia (au kusimamia?) kipindi cha mpito. Pia alikuwa anafikiria kurudia yale aliyofanya mwaka wa 1962 alipojiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu. Alihisi kulikuwa na vuguvugu ya chini kwa chini katika chama chake cha TANU. Mara baada ya uhuru waliopewa nyadhifa za serikali walikuwa wasomi. Sasa viongozi wa chama ambao waliojitolea kwa hali na mali katika mapambano ya ukombozi waliachwa. Walinung’unika. Wakaona sio haki waliochangia katika mapambano ya uhuru wasifaidike na matunda ya uhuru wakati waliokuwa na mchango mdogo wanufaike. Mwalimu karajea chamani kutuliza vuguvugu pamoja na kupanga fursa, kwa mfano, za wakuu wa mikoa  na wilaya kwa ajili ya viongozi hao wa chama ambao hawakuwa na elimu ya juu. 

Baada ya miaka takriban arobaini sasa akataka kurudia alichokifanya 1962. Safari hii kazi aliyonayo ilikuwa ni kuchunguza hali ya chama na kuiimarisha ili kiweze kusimamia ujamaa. Akaanza ziara zake za mikoani na wilayani. 

Huko mikoani na matawini alikuta nini? Alishangaa na kushtuka kuona chama hakikuwa katika hali aliyotarajia. Chama hakikuwa tena na ule ushawishi na shauku ya ukombozi. 

Wanachama walikuwa wakilalamika. Wakamueleza Mwalimu wazi wazi kwamba chama chake kilitekwa nyara na warasimu wenye uchu wa madaraka. Viongozi wa chama waligeuka kawa mabosi na waheshimiwa; sio tena ndugu. Hawakujali wananchi na kero zao. 

Mwanzoni Mwalimu alijaribu kuwatetea viongozi wa chama chake lakini hatimaye kakata tamaa. Aliwaachia wananchi wazungumze na hapa na pale kuwasimamisha viongozi kuwajibu wanachama. 

Pole pole Mwalimu kaanza kuelewa kwamba katika utawala wake wa miongo takriban minne chama kilijijengea urasimu na protokali ya serikali. Kikageuka kuwa chama-dola (state party) badala ya chama cha ukombozi. Kwa kiasi fulani Mwalimu mwenyewe hawezi kuepuka lawama. Chini ya usimamizi wake nyadhifa za serikali na za chama zilichanganywa. Chama kikakijengea urasimu wake. Ninakumbuka wakati moja Mzee Pius Msekwa akiwa Katibu Mtendaji wa chama aliwahi kuandika nyaraka kupendekeza chama kuwa na utumishi wake wa chama kama utumishi (civil service) wa umma. Hayo yote yalifanyika chini ya kauli mbiu ya chama kushika hatamu. Dhana ya chama kushika hatamu hakikuwa na maana ya chama kuingoza serikali na umma kifalsafa na kiitikadi. Chama kushika hatamu ukageuka kuwa viongozi kushika utamu!  

Katika hali hiyo na mazingira hayo je Mwalimu kweli angeweza kubadili chama chake na kukirejesha katika mtazamo wa kijamaa na ukombozi? Inaelekea Mwalimu hakutaka kukata tamaa. Alijiamini sana. Ukaidi wake ulimfanya Mwalimu bado awe na matumaini ya kurekebisha chama pamoja na dalili zote kudhirisha kwamba mazingira hayakuwa rafiki. Viongozi wenzake wenyewe hawakuwa na shauku ya ujamaa. Wananchi walichoka na maisha magumu. Walikuwa na tamani ahueni mara moja. Ingawa Mwalimu alibaki na heshima zake na upendo wa umma kwake, umma haukuwa tayari kujitosa tena mara ya pili katika majiribio mapya ya aina yoyote ile. 

Pamoja na ukweli huo Mwalimu kagombea tena uenyekiti wa chama 1987 kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Lakini hakumaliza kipindi chake cha pili. Mnamo mwaka 1990 kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi kaachia ngazi ya uenyekiti. Kuna mambo makubwa yaliyotokea kati ya 1987-1990 kumfanya Mwalimu asimalize kipindi chake cha pili cha uenyekiti. 

Nitayazungumzia hali ilivyo katika kipindi hiki cha 1987-1990 nchini na duniani katika barua yangu ijayo. 

Wasalaam

Issa

3 responses to “5 BARUA YA Wiki kwa mpendwa wangu azimio”

  1. Swadakta

    Like

  2. Asante kwa maarifa prof

    Like

  3. asante sana Ndugu Profesa Emeritus issa::: nafurahi kufuatilia makala:: pia kuna speech moja uliitoa wakati wa uzinduzi wa kigoda cha Mwal ulikuwa wewe na ndugu jeneral ulimwengu natamani nipate hizo hotuba

    asante wako

    Aloyce

    Like

Leave a comment

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags