24/03/2024
Mpendwa Azimio
Hii ni barua yangu ya saba kwako. Sikumbuki kama nilikutaarifu kwamba nimeweka barua hizi hadharani kwa ajili ya vijana kuzisoma na kuelewa tulikotoka na tulipo. Kwa maoni yangu, huwezi kuelewa ulipo kama hujui ulikotoka na huwezi kuelezea yaliyopo kama hujui yaliyokuwepo. Lakini sina uhakika kama vijana wanazisoma barua hizi. Aah! Lakini bila kujali kama wanazisoma au hawazisomi ni wajibu wangu kuendelea na simulizi ya historia yetu.
***
Kipindi cha pili cha awamu ya pili chini ya Mzee Mwinyi kilishuhudia mambo matatu makubwa katika historia yetu ambayo yaliashiria kuingia kwa mfumo wa uliberali mamboleo na kuachana na enzi ya utaifa na uzalendo chini ya Mwalimu Nyerere. Kwa hakika, awamu ya Mzee Mwinyi ilikuwa ni kipindi cha mpito kati ya utaifa (nationalism) na uliberali mambo leo (neoliberalism).
Mwinyi alishinda kwa kishindo uchaguzi wa 1990. Katika hotuba zake za kempeni alisisitizia sana ahueni aliyoletea wananchi kwa kufungua milango ya uchumi; kulegeza masharti ya biashara na kuruhusu wafanyabiashara kuagiza na kuingiza bidhaa bila masharti. Hata ilani ya CCM ya uchaguzi haikugusia mambo ya Azimio la Arusha. Hii peke yake ni dalili tosha ya kuonyesha kwamba warithi wa Mwalimu walikuwa mbioni kuzika Azimio la Arusha.
Mwinyi akamteua Mzee Malecela kama Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa rais. Na akamteua hayati Horace Kolimba kuchukua nafasi ya Mzee Kawawa kama katibu mkuu wa chama. Mzee Kawawa kawa makamu mwenyekiti wa chama, wadhifa isiyona mamlaka makubwa. Sina hakika kama Mwinyi alifanya uteuzi hizi kwa kushauriana na Mwalimu.
Mara baada ya uchaguzi Halmashauri ya Chama iliyokutana Zanzibar ikapitisha azimio kufuta masharti na miiko ya uongozi. Sasa viongozi wa chama na serikali walikuwa huru kujitajirisha na kujilimbikizia mali kwa njia mbalimbali – kuanzisha biashara zao, kununua hisa katika makampuni binafsi, kukodisha nyumba zao n.k. Mwalimu alikuwa anashuhudia mambo haya yote bila kusema chochote. Hakuzungumzia Azimio la Zanzibar kwa takriban miaka mitano. Kama alisikitika basi alisilitika kimyakimya moyoni mwake.
Jambo la pili lilikuwa kupitisha sheria rasmi kuhusu mfumo wa vyama vingi 1992 baada ya Tume ya Jaji Nyalali kupendekeza hivyo. Sio viongozi wengi wa chama walitaka au kufurahia vyama vingi. Kwa mfano, rais wa Zanzibar wakati ule Kamando Salmin Amour hakutaka kabisa mfumo wa vyama vingi lakini asingeweza kupinga uamuzi wa chama. Akakubali shingo upande. Ukweli ni kwamba ilikuwa shinikizo la Mwalimu kufanya mageuzi katika mfumo wa vyama. Mwalimu alikuwa na sababu mbili. Moja aliweka wazi. Hoja yake iliegemea mabadiliko duniani na kusambaratika kwa nchi za kijamaa ambazo zilikuwa zinafuata mfumo wa chama kimoja. Mwalimu alirudiarudia kusema kwamba kama sisi wenyewe hatutabadili mfumo wa vyama tutalazimishwa kuubadilisha kutokana na shinikizo za nje.
Sababu ya pili ambayo hakuweka wazi ilikuwa kwamba CCM ilikuwa inahitaji upinzani madhubuti ili isiendelee kulegalega. Ingawa pia aliamini kwamba upinzani thabiti ungetokea CCM chenyewe. Ingawa hakusema lakini kuna dalili kwamba alikuwa anatamani baadhi ya viongozi wa CCM wangeanzisha chama chao ambacho angependelea kuwa chama cha kijamaa. Nitarejea suala hili hivi punde.
Jambo la tatu ni lile la G55 la kupitisha azimio Bungeni likitaka kuanzishwa kwa Tanganyika katika Muungano. Wabunge wa CCM takriban 55 walipendekeza na hatimaye azimio la Bunge likapitishwa likiagiza serikali kuleta muswada wa sheria kuwa na serikali ya Tanganyika katika Muungano. Kimsingi, hili halikuwa lingine isipokuwa kuwa na muungano wa serikali tatu. Suala la kuwa na muungano wa serikali tatu liliibuliwa mara ya kwanza mnamo 1983 na hayati Aboud Jumbe ambalo ilipelekea kwenye kile kilichoitwa machafuko ya hali ya siasa. Muundo wa serikali tatu ulipigwa vita na Mwalimu. Katika mkutano wa Halmashauri ya Chama ulioitwa rasmi kuyajadili machafuko ya hali ya siasa Mzee Aboud Jumbe alishambuliwa sana, shambulizi likiongozwa na hayati Seif Sharif Hamad. Hatimaye Jumbe alilazimika kujiuzulu nyadhifa zake zote za serikali na chama.
Safari hii tena Mwalimu akapinga kwa nguvu zake zote azimio la G55 akilaumu Waziri Mkuu Malecela na Katibu Mkuu Horace Kolimba kumshauri Mwinyi vibaya kiasi kwamba azimio likapitishwa. Hoja ya Mwalimu ilikuwa kwamba muungano wa serikali mbili ilikuwa sera ya Chama na wabunge wote waliyoingia bungeni kwa tiketi ya Chama walitakiwa kutetetea muundo huu wa Muungano. Sera ingebadilishwa tu kwa ridhaa ya wanachama wa Chama. Kwa mantiki hii hatimaye azimio lilizimwa baada ya idadi kubwa ya wanachama kupigia kura kuendelea na muundo wa serikali mbili.
Hata hivyo Mwalimu alikuwa anakutana na kundi la G55 na kujadili nao azimio lao bila hasira. Ndio wakati huu Mwalimu alitamani wabunge hao vijana wangejitenga na CCM na kuanzisha chama chao wakiwa na hoja nzito kuliko ile ya serikali tatu.
Ni vema kujikumbushia kwamba upinzani mkali wa Mwalimu dhidi ya serikali tatu ni hofu iliile ya kusambaratika kwa nchi. Wakati wa vuguvugu la G55 Mwalimu aliandika shairi ndefu iliyochapishwa nje ya nchi. Kwa ustadi mkubwa na hisia mkali Mwalimu alirudia hoja zake dhidi ya mfumo wa serikali tatu akiwalaumu sana Malecela na Kolimba (lakini sio Mwinyi wala kundi la G55) akiwalinganisha na Boris Yeltsin wa Urusi aliyesimamia kuvunjika kwa Soviet Union.
Nimalizie kwa kurejea kwenye hoja yangu kwamba awamu ya Mzee Mwinyi ilikuwa ni kipindi cha mpito kuelekea mfumo wa uliberali mambo leo. Pamoja na kulegeza masharti ya biashara na kuondoa uthibiti wa karibu wa shughuli na sera za fedha, pia chini ya usimamizi wake ilipitishiwa sheria kuwezesha ubinafsishaji wa mashirika ya umma, mchakato ambao aliendeleza na kuyakamilishi hayati Rais Mkapa katika awamu ya tatu.
Sitakosea kusema Mzee Mwinyi mwenyewe hakuwa muumini wa dhati wa ujamaa. Hata uzalendo wake ulikuwa wa kusuasua.
Wasalaam
Issa



Leave a reply to Logic Malyangu Cancel reply