31/03/2024
Mpendwa Azimio
Kama awamu ya Mzee Mwinyi ilikuwa kupanda mbegu za uliberali mamboleo, basi awamu ya hayati Mzee Mkapa ilikuwa ya kukamilisha ukuaji wa uliberali mamboleo. Ubinafsishaji wa mashirika ya umma, na kwa jumla, kuondoa umilikaji na uthibiti wa uchumi na serikali ni agizo mojawapo la wapigadebe – taasisi za fedha za kimataifa na nchi za kibeberu – wa uliberali mamboleo. Pamoja na soko huria ubinafsishaji na ubidhaaifishaji (commodification) wa kila kitu ni nguzo muhimu ya mfumo wa ubepari ambao tunauita uliberali mambo leo. Mzee Mwinyi alikita zaidi kwenye soko huria. Mzee Mkapa kwa upande wake akaharakisha kwa kasi kubwa ubinafsishaji. Kama soko huria ikawa soko holela basi ubinafsishaji ukawa ufujaji na ubadhirifu wa mali ya umma.
Zaidi ya asilimia hamsini ya mashirika ya umma yalibinafsishwa kwa bei poa bila kujali unyeti wao katika uchumi wetu. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo ilikuwa benki pekee yenye mtandao wa matawi nchi nzima iliuzwa kwa kampuni ya Afrika Kusini, ABSA. Reli ya kati ilitakiwa iendeshwe na mashirika ya nje. Mitambo ya kusafisha petroli (TIPER) iliuzwa kwa Oryx ambayo haikuona maslahi kuendesha mitambo. Wakaiuza na kugeuza kiwanda kuwa maghala. Ndivyo tukawa tegemezi kununua petroli kutoka soko la kimataifa. Uwezo wetu wa kudhibiti bei za mafuta kwa kuhifadhi petrol na kuweka sokoni wakati bei zinapanda ukatoweka. Tukatupwa moja kwa moja katika soko la kimataifa. Mpaka leo tunaendelea kuathirika kila mara bei za petroli zinapanda. Tusijidanganye. EWURA haina uwezo wowote wa kudhibiti bei za petroli.
***
Hakuna yeyote, sio vyama vya siasa wala mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), sio wasomi wala wanasiasa, walipinga ubinafsishaji holela. Waliopinga walikuwa wafanyakazi. Wafanyakazi wa NBC, wafanyakazi wa Reli, wafanyakazi wa TIPER wote walipeleka upingamizi wao mahakamani na kupata amri za zuio (injunction) wakitaka haki zao zieleweke na kuwekwa wazi. Mkapa alikasirika sana. Aliwahi kusema kwamba kama angekuwa na uwezo angepiga marufuku amri ya zuio. (Kwa hulka yake Mkapa alikuwa mwepesi kukasirika.)
Wafanyakazi pia walikuwa waathirika wakubwa wa ubinafsishaji kwa kupoteza ajira katika mchakato wa upungzwaji wa wafanyakazi na wamiliki binafsi. Maelfu ya wafanyakazi na familia zao wakapoteza riziki yao. Wengi walipoteza muda mwingi tu wakifuatilia mafao yao – baadhi wakafariki kwa ugonjwa au mishtuko hata kabla ya kupata haki zao.
***
Mzee Mwinyi kaondoa miiko ya viongozi. Mzee Mkapa akawauzia nyumba za serikali kwa bei za kutupa. Baadhi ya hao viongozi waka karabati hizi nyumba kwa gharama za serikali. Gharama za kukarabati zilikuwa kubwa kuliko bei waliotoa kununua hizi nyumba.
Ilikuwa pia nyakati hizi sheria ya madini ikapitishwa. Sheria hii ilitoa uhuru mkubwa kwa wawekezaji katika migodi. Chini ya Mkapa na Chenge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali enzi ya Mkapa, wakairekebisha Katiba ya nchi kwa kuitafsiri rasmi dhana ya ujamaa. Tafsiri yenyewe ikapoteza kabisa maana ya ujamaa; ndio hasa ilikuwa lengo lake. Ibara ya 151 inasema kwamba maana ya ujamaa au ujamaa na kujitegemea ni
“misingi ya maisha yajamii ya kujenga Taifa linalozingatidemokrasia, kujitegemea, uhuru,haki, usawa, udugu na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano”.  Sasa chini ya tafsiri hii nani asiye mjamaa au nchi gani sio nchi ya kijamaa! Hata Marekani inaweza ikadai ni nchi ya kijamaa chini ya tafsiri hii ya ujamaa.
Kabla ya hii hatukuwa na haja ya tafsiri kwa sababu kila moja wetu tulitambua ujamaa kwa sifa zilizowekwa katika Azimio la Arusha.Â
Ni vema kuweka jambo moja katika kumbukumbu. Kwa kuwa Mkapa alikuwa kutoka kizazi kile cha viongozi kilichofanya kazi karibu na Mwalimu na walijua tamaduni za Chama tawala. Hivyo, Mkapa aliendelea na utamaduni wa vikao vya Chama ambavyo vilijadili mambo muhimu ya sera na mielekeo ya serikali. Pamoja na hilo, Mkapa alikuwa mkali, kwa hivyo, aliweza kuwadhibiti mawaziri wake. Hili lilikuwa tofauti na awamu ya nne iliyofuata ambayo tutaizungumzia katika barua ijayo. Katika awamu ya nne chini ya Mheshemiwa Kikwete, kwa lugha ya kimombo, “neoliberal chickens came home to roost.”
Wasalaam
Issa



Leave a reply to pharm Adimin Cancel reply