11 barua ya kila wiki kwa mpendwa wangu azimio

21/04/2024

Mpendwa Azimio

Rais wa sita Mhe. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani  aliamsha matumaini mapya. Watu walipumua baada ya uhuru wao kubanwabanwa chini ya rais wa tano.  Viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma, wafanyabiashara walitarajia ahueni. Nchi za kibeberu na makampuni yao hawakupoteza muda kujipenyeza karibu na rais mpya. 

Wanyonge na matabaka ya chini je? Wao hawakuwa na uhakika; mashaka yao yaliendelea. Uzoefu wao uliwafundisha kuwa yakitokea mabadiliko katika ngazi za juu, waathirika wa kwanza ni wao. Mara baada ya Mama kushika hatamu, nilitunga utenzi ulioitwa ‘Mamangu Tanzania’. Beti ya mwisho ilisema:

Bintiye kakuahidia suluhu na (akina) Uhuru

Kakutuliza kwa kufungulia vidirisha vya kupumua 

Na vyombo vya kuburudisha

Mamangu Mpendwa unanisumbua kwa kunipigia simu kila kukicha:

‘Je bibiye atafungua pia

Mabomba ya maji machafu?’

‘ Je bibiye atafungua pia

Mabomba ya maji machafu?’ ndio mada ya barua yangu. 

***

Kwa kuwa Rais wa sita amekuwa madarakani miaka mitatu tu, nitazungumzia mielekeo tunachoshudia na kutoa angalizo, (kwa maoni yangu) pale inapostahili. 

Kwanza, hakuna shaka kwamba uwanja wa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari umerejeshwa. Isipokuwa kwa upande wa vyombo vya habari inaelekea hawataki kujitosa kwenye kutoa taarifa na uchambuzi wa kina utakaoudhi serikali na waheshemiwa. Hivyo, wimbo wa kusifiwa Mhe. unaendelea tena kwa kasi. Kwa kweli, vyombo vyetu wa habari, ukiachilia vichache ambavyo havina mvuto mkubwa, vimeendelea kuwa watiifu mno kwa wenye madaraka. 

Kwa upande wa wanasiasa, hasa wa upinzani, wamefunguliwa milango ya kufanya siasa ingawa bado wanajikuta wanakwamishwa hapa na pale. Pamoja na hayo, kuna dalili zimejitokeza hivi karibuni kwamba milango ya uhuru inaweza ikafungwa na wale wanaojiita wachawa. Popote pale, hata katika nchi zinazodai kuwa nchi za kidemokrasia, uhuru hauwezi kuchukuliwa kana kwamba hauminyiki. Uhuru ni uwanja wa mapambano. Lazima upambaniwe. Lazima ulindwe. 

Pili milango ya uwekezaji kutoka nje imefunguliwa bila uthibiti wowote. Aina ya uwekezaji na maeneo ya kuwekeza inaelekea ni kwa utashi wa wawekezaji na sio kwa mujibu wa mpango wa nchi. Wao ndio wanaopanga ajenda, sio sisi. Tumeshudia wafugaji wa Ngorongoro wakihamishwa na ardhi yao kutwaliwa kwa visingizio mbalimbali lakini ukweli unabaki pale pale. Ni kwaajili ya makampuni ya uwindaji, mengi kutoka Urabuni. 

Hivyo vilivyo katika sekta nyeti ya bandari. Tumekabidhi bandari yetu ya Dar es Salaam kwa kampuni ya Ufalme wa Kiarabu bila kufikiria athari zake kwa wananchi hasa kwa ajira, ardhi na usafiri. Tuwe macho. Hii kampuni ya DP World inaweza ikawa na malengo zaidi ya kuendesha bandari. Inataka kujipenyeza katika uchumi wetu. Tusije tukajikuta tunakuwa waathirika mithili ya hadithi ya Mwarabu na ngamia. Mwarabu kwa mwema wake kamruhusu ngamia kuweka mgu  wake ndani ya hema ili asiteseka na baridi. Hatimaye akajikuta kapigwa teke na ngamia na kufukuzwa moja kwa moja nje ya hema. 

Inaelekea tumeanza mchakato wa ubinafsishaji bila kutathmini kwa undani ubinafsishaji wakati wa awamu ya Mzee Mkapa. Ubinafsishaji wa kiholela unaweza kuathiri vibaya uchumi wetu na huduma kama usafiri, umeme, nishati, maji n.k. kwa wananchi wetu. 

Tatu ni mikopo. Katika miaka mitatu iliyopita tumekopa sana bila kikomo. Mwishoni mwa 2020 (Disemba 2020) deni la  taifa lilikuwa shillings 59 trillion. Mwishoni mwa 2023 (Disemba 2023) lilikuwa shilingi 87.4 trillion. Katika miaka mitatu deni limeongezeka kwa takriban asilimia 28.5. Fedha iliyotengwa katika bajeti ya serikali ya 2023/24 kulipa deni ilikuwa shilingi 10.48 trilioni zaidi kidogo ya fedha zilizotengwa kwa sekta tatu ya elimu, afya na kilimo.  Hii ina maana tunalipa zaidi kurudisha deni kuliko kuboresha sekta zetu muhimu ya uzalishaji (kilimo) na sekta za huduma (afya na elimu).  Tusisahau kwamba deni ni mtego. Ukishaingia  kwenye mtego wa deni ni vigumu kujiokoa. Ni  sawa na kuingiza  mkono wako mdomoni wa papa. Atakumeza tu. Ndio hulka ya papa ya kifedha (financial sharks).  Wakifanikiwa kukunasa katika mtego wa deni utajikuta unaendelea kukopa ili  kurejesha mikopo ya awali. 

Nne, mazungumzo miongoni mwa wananchi wa hali ya chini na hata wafanyabiashara ni kwamba rushwa, hongo na ubadhirifu wa mali ya umma  umeongezeka ukilinganisha na awamu ya hayati Magufuli. Matumizi ya anasa ya viongozi wa serikali na watumishi wa umma unaonekana wazi wazi. Magari wanayotembea nayo, hoteli za kifahari wanakofikia, idadi ya masemina wanaoanda, safari za nje za mara kwa mara,  haya yote inagharimu serikali – ni fedha kutoka jasho la wananchi. 

Katika nchi ambako wananchi wengi wamezama katika dimbwi la umaskini, viongozi wakiishi maisha ya kianasa inazaa uchuki unaosubiri kulipuka. Tuepukane na hilo. 

Mwishowe, nigusie jambo ambalo limeniaibisha sana mimi binafsi. Na hii ni mtazamo na mwelekeo wetu wa mahusiano na nchi za nje. Mwalimu Nyerere alituwekea misingi ya sera yetu ya nje. Kwanza kusaidia ukombozi wa nchi za Afrika kutoka ukoloni. Na hii ni pamoja na ukoloni wa ndani. Ndio maana alitetea haki ya Wasahrawi kuwa na nchi huru na alipinga Morocco kuendelea kutawala eneo la Sahrawi. Pili ni kuunganisha nchi za Afrika, umoja wa Afrika, ili kuweza kupambana na ukoloni mambo-leo.  Tatu, popote pale  penye dhuluma na ukandamizwaji sisi kama nchi tulisimama kwa upande wa wanyonge.  Ndio maana tulikuwa tunaunga mkono ukombozi wa Wapalestina dhidi ya nchi dhalimu ya Israel.  Nne, tulikuwa na uhusiano wa kirafiki na nchi za Ulaya zenye mrengo wa kimaendeleo (Progressive) kama nchi za Scandinavia. Tano, tulikuwa waangalifu sana  katika uhusiano wetu na nchi za kibabe (superpowers) hususan Marekani na Soviet Union. 

Sasa leo hii mtazamo wetu kuhusu sera ya nje ni nini? Tumeyakumbatia nchi za kibeberu bila kuhoji athari zake.  Msimamo wetu au kutokuwa na msimamo juu ya mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza unatusibisha mbele ya jumuiya ya kimataifa. Ukimya wetu umekuwa wa kutisha. Hata hatukuunga mkono Afrika ya Kusini katika kesi dhidi ya Israel waliyopeleka Mahakama ya Kimataifa. Mbaya zaidi hatukuruhusu hata wananchi wetu waonyeshe hisia zao kwa maandamano au makongamano. Ni aibu tupu. 

Vijana wetu wamebaki wakidwaa. Hii kweli Tanzania yetu tunayosoma vitabuni!  

***

Mpendwa Azimio. Naamini umesitisha kususia kwako. Juzi ukaja ndotoni mwangu. Ulinipa darasa. Nimekariri neno kwa neno uliyoniambia. Nitayazungumzia mawaidha yako katika barua ijayo. 

Wasalaam

Issa

One response to “11 barua ya kila wiki kwa mpendwa wangu azimio”

  1. Maarifa mujarabu

    Like

Leave a reply to Maiko Mwageni Cancel reply

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags