5/05/2024
Mpendwa Azimio
Katika barua hii nitaendelea na simulizi yako. Niwie radhi. Ulichoniambia ni muhimu mno. Sianabudi niendelee kushare na wajukuu wako.
‘Kama nilivyokueleza; pamoja na wafanyakazi, wakulima walikuwa tabaka lingine lililoainishwa katika Azimio la Arusha kama tabaka la msingi. Yaani, wakulima na wafanyakazi walichukuliwa kama wajenzi na hatimaye wanufaika wa Ujamaa. Nyaraka juu ya Ujamaa Vijijini iliyoweka maono na mtazamo wa maendeleo vijijini iliandikwa na Mwalimu mwenyewe. Ni baadae ndio chama kilirasmisha na ikawa nyaraka ya Chama pamoja na Azimio la Arusha.
Kabla sijaendelea nitie neno juu ya vijiji vya Ujamaa viliyoanzishwa huko Songea na vijana wa TANU Youth League mara baada ya uhuru chini ya uongozi wa Ntimbanjayo Millinga. Kijiji cha kwanza kabisa kilikuwa Litowa. Hatimaye vijiji kama 11 vilijirasmishwa chini ya jumuiya iitwayo Ruvuma Development Association au RDA. Vijiji hivyo viliendeshwa kwa msingi wa kijamaa kweli kweli. Walikuwa wanalima kwa pamoja. Walikuwa wanafanya maamuzi yao kwa pamoja. Walikuwa na shule yao ya kijiji. Jinsi shule ilikuwa inaendeshwa ikawa mfano wa kuiiga. Mwalimu mwenyewe kaandika nyaraka yake Elimu ya Kujitegemea kwa kutumia misingi iliyowekwa na Shule ya RDA. Kila mara Mwalimu alitumia mfano wa vijiji vya RDA kwa kuelezea falsafa yake ya Ujamaa vijijini.
Lakini warasimu wa serikali katika ngazi ya mkoa na hata wajumbe wa Kamati Kuu ya chama (TANU) walichukuia sana RDA kutokana na mafanikio na mfano wake hasa kwa sababu RDA haikuwa chini yao. Chombo chochote kile ambacho kilikuwa huru na kujiendesha chenyewe kwa kujitegemea kilionekana kama adui wa hao wamangimeza. Hatimaye baada ya uhasama wa muda mrefu na baada ya mjadala mkali katika Kamati Kuu ya Chama RDA ikapigwa marufuku. Mwalimu kashindwa kuitetea RDA na kuilinda. Badala yake kameza uamuzi wa Kamati Kuu na kuihalalisha kwa kusema kwamba Ujamaa vijijini ilikuwa sera ya Chama. Kwa hivyo, ingetekelezwa na Chama chini ya usimamizi wake. Kama alivyoua vuguvugu la wafanyakazi kutoka chini, ndivyo alivyoua vuguvugu la wakulima kujenga vijiji vyao kutoka chini. Mwalimu kafanya kosa lingine la kihistoria.
Nirejee kwenye simulizi yangu.
Tangu awali mtazamo wa sera ya Ujamaa vijijini ulikuwa kwamba wakulima wasilazimishwe kujiunga na vijiji vya Ujamaa; kwamba washawishwe kujiunga kwa hiari yao. Ujamaa hauwezi kulazimishwa, Mwalimu alirudiarudia kusema. Baada ya muda walipokuta kwamba kasi ya kuanzishwa kwa vijiji vya Ujamaa ilikuwa ndogo mno, Viongozi wa Chama na warasimu wa serikali wakapoteza uvumulivu. Kila kiongozi wilayani na mkoani alitaka kuonyesha idadi kadha ya vijiji vya Ujamaa katika eneo lake. Na hawakusita kutumia nguvu. Wakamshinikiza Mwalimu. Mara nyingine tena Mwalimu akaenda na ushawishi wao. Akatangaza rasmi Operesheni Vijiji. Mwalimu katoa agizo: kuishi vijijini si hiari, ni lazima. Ingawa vijiji sasa vikaitwa vijiji vya maendeleo. Wakipenda wasipende wakulima lazima wahamie vijijini viliyopangiwa rasmi. Operesheni Vijiji ikaendeshwa kama Operesheni ya kijeshi.
Kwa mabavu na ukatili mkubwa mamilioni wa wakulima na wafugaji walisombwa na malori kupelekwa vijijini. Mabavu yakatumika. Wengi waliumia. Wengine walifariki. Mazao yao yalifekwa. Makazi yao yalichomwa. Inakadiriwa watu takriban milioni tano walihamishwa katika miaka kama minne hivi. Hata baada ya kukiri kwamba baadhi ya wananchi waliumizwa, Mwalimu katangaza operesheni vijiji ilifanikiwa na kuwapongeza watendaji wake.
Kama alivyopoteza ushabiki wa wafanyakazi, ndivyo Mwalimu kapoteza imani ya wakulima kwake. Kosa lingine la kihistoria. Walinzi na watetezi wa Ujamaa, wakulima na wafanyakazi, wakageuzwa kuwa wachukiaji wa Ujamaa!’
Labda kunituliza, ukaendelea kwa sauti yako nyororo:
‘Issa maskini
Kulikoni?
Vipi Issa Bin Mariam?
Hukutambua
Mpendwa wako
Mjamaa wa kupindukia
Kawa chanzo
Cha wakulima na wafanyakazi
Kuchukia Ujamaa.’
Mpendwa Azimio nilikuwa nakusikiliza kwa makini sana ingawa mengine yalinichoma. Nikasema moyoni: Duh! mpendwa wangu anaweza kumkosoa mlezi wake bila kuminya maneno!
Hata hivyo, nimejifunza mengi. Nikajifunza kujikosoa na kukosoa wapendwa wangu bila upendeleo. Nitaendelea kujifunza.
Katika barua ijayo nitashare na wajukuu wako somo mojawapo la kipekee uliyoniachia – somo la umuhimu wa kuwa na chombo huru cha wavujajasho wenyewe katika kuendeleza mapambano yao.
Wako
Issa



Leave a comment