15 barua ya kila wiki kwa mpendwa azimio

19/05/2024

Wapendwa Wajukuu wa Azimio

Hii ni barua ya mwisho katika mfululizo wa barua ya kila wiki kwa Azimio. Natumai tumejifunza mengi kutokana na simulizi ya sifa muhimu za awamu zote za marais sita na hasa kutokana na ukosoaji mkali wa Azimio mweyewe. 

Kabla sija anza kuzungumzia mafunzo tuliyoyapata,  napenda nisisitize jambo moja. Kamwe tusisahau wala kulibeza awamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mchango wa Mwalimu katika kutujengea heshima hauna ulinganishi. Mwalimu ndio aliyetujengea utambulisho wetu wa kitaifa (national identity). Mpaka leo tunajivunia Utanzania wetu. Vijana wetu wanaweza wakatembea popote pale duniani na kifua mbele; sio wanyonge tena. Mwalimu ndio alisisitiza sana elimu na kaweka msingi wa elimu ya juu. 

Maadilili, uledi na uadilifu wa Mwalimu ni mfano bora barani Afrika. Ni Kiongozi ambaye asingeweza kunyumbishwa au kununuliwa. Alikuwa na msimamo thabiti na maono mapana. Alikuwa anawazia hatma ya nchi yake na watu wake miaka hamsini kabla ya wakati. Fikra zake zilikuwa za masafa marefu. Pamoja na mapungufu na makosa yake; pamoja na ukweli kwamba vitendo vyake vingine havikuendana na msimamo wake wa kustawisha maisha ya wanyonge, hakuna mtu, hata adui wake, ambaye angeweza kutilia mashaka nia yake na ukweli kwamba hakukuwa na chembe ya ubinafsi. Kwa hivyo, anastahili kuenziwa na kulindiwa heshima zake zote na uadilifu wake uliotukuka. 

Wapendwa wajukuu wa Azimio: kamwe msikubali kupotoshwa kuhusu Mwalimu. Pingeni wale wanaotaka kumshetanisha Mwalimu. Mwalimu hakuwa malaika lakini alikuwa binadamu safi.  He was a great leader by any standard.  

***

Kwa muhtasari tu nitazungumzia machache tuliyoyapata kutoka barua hizi. Kwanza kabisa narudia kusisitiza umuhimu wa kujua historia yetu. Barua hizi zimegusia mambo machache tu. Someni historia yetu. Mkijua historia ya nchi yenu vizuri, hamtaweza kumezeshwa propaganda za kisiasa. Msisahau kwamba kila utawala  unatengeneza historia kwa mtazamo wao wenye maslahi kwao. Kamwe msichukulie wazo-tawala kama wazo sahihi asilimia mia moja. 

Pili, wakereketwa wa mrengo wa kushoto wenye mtazamo wa kiproletari hawanabudi waelewe na kukariri ukweli kwamba ukombozi wa wavujajasho ni jukumu la wavujajasho wenyewe na sio zawadi ya kiongozi wa dola au masiha. Dola hatimaye ni chombo cha tabaka tawala. Wasilitegemee. Wajitegemee. 

Tatu, matabaka ya chini hayanabudi kujijengea chombo chao cha kuwatetea na kuwalinda. Chombo chao ni nguvu yao. Chombo ndicho kinawaunganisha na kutatua migongano ya ndani (internal contradictions). Bila kuwa na chombo, watawala wanatumia migongano na misuguano miongoni mwa wavujajasho kuwagawanya. 

Mwisho, ni jukumu na wajibu wetu kama wanazuoni kujielimisha na kujipatia maarifa ya kuchambua kwa ustadi hali halisi ili tuweze kuwasaidia wanyonge kufumbua macho yao ili waweze kutambua ukweli na uongo. Yaani waweze kutambua nini ni makapi na nini ni mchele. 

Natumai wasomaji watakuwa na maoni yao. Nawakaribisha kupost yao kwenye issashivji.com

***

Kama nilivyosema mwanzoni, hii ni barua ya 15 na ya mwisho katika mfululizo wa barua ya kila wiki kwa Azimio. Kuanzia wiki ijayo nitaanza mfululizo mpya, mfululizo wa Mazungumzo ya Kufikirika. 

Wasalaam

Issa

5 responses to “15 barua ya kila wiki kwa mpendwa azimio”

  1. Fransisco John Avatar
    Fransisco John

    um

    Like

  2. Fransisco John Avatar
    Fransisco John

    Umejaa maarifa makubwa wewe ni hazina kubwa ya watanzania inayotembea endelea kuwafumbua macho watanzania

    Like

  3. Maiko Mwageni Avatar
    Maiko Mwageni

    asante Sana kwa maarifa prof,,SASA tuandike hali halisi ya siasa na uchumi

    Like

  4. asante sana, kazi yako ni njema sana.

    Like

  5. Mawasiliano yamefanyikw kwa USTADI mkubwa. Hakika ubobezi uliotukuka unajidhihirisha wazi katika mantiki za barua hizi. Hongera sana Prof.

    Tunatarajia “madini” ya kutosha katika ‘episode ya Kufikirika’ itatuamsha kuelekea mtazamo chanya wetu na vijana wetu mustakabali wa vizazi vijavyo InshaAllah!

    Like

Leave a reply to qwyckg Cancel reply

Hey!

I’m Bedrock. Discover the ultimate Minetest resource – your go-to guide for expert tutorials, stunning mods, and exclusive stories. Elevate your game with insider knowledge and tips from seasoned Minetest enthusiasts.

Join the club

Stay updated with our latest tips and other news by joining our newsletter.

Categories

Tags