26/05/2024
Tanzanite: (kwa sauti ya kejeli) Enhe “rafiki” yangu. Umetupwa wapi, katika stoo gani huko barabara ya mlezi wako, eti barabara ya Nyerere, baada ya kuondoshwa kutoka daraja la Tanzanite!?
Mwenge: Popote pale nilipo nitaendelea kutoa mwanga. Mwanga wangu unaweza kufifia lakini kamwe hauta zimika.
Tanzanite: Acha kiburi chako. Wala haijulikani ulijipenyeza je huko daraja la Tanzanite. Sio hadhi yako.
Mwenge: Weka hadhi yako mfukoni mwako. Mie ninaheshima zangu mioyoni mwa watu. Unahabari? – madereva wa dala dala walikuwa wanani salimu kwa kunipigia honi kila wakipita. Wewe je!
Tanzanite: Mimi sio kasichana ka barabarani nitongozwe na honi ya kila hohehahe, wapita njia muflisi. Mimi ni mrembo mashuhuri. Ninasafiri kwa ndege na helikopta kwenda kurembesha wake za akina Bill Gates na malaika wa Uarabuni.
Wewe hata kuvuka mipaka hujawahi kuvuka, sembuse kuruka na ndege.
Hata huko darajani nilitua na helikopta. Na wewe ulikuwa unabebwa mgongoni mwa vijana kama mtoto mchanga.
Mwenge: Acha kujigamba. Eti mrembo! Mrembo gani wakati hata kumeremeta unashindwa mpaka umekatwa katwa kama kuku na kufanyiwa operesheni kuwekewa taa tumboni mwako.
Uzuri wangu ni wa asili. Hauhitaji kutangazwa. Mwanga wangu ni kumulika njia sio kuwavutia watalii. Nilipata heshima kuwekwa Mlima Kilimanjaro ili kuleta ‘tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dhaarau.’
Tanzanite: Ah! Wewe bwana una maneno mengi, wala sikuelewi ….
Mwenge: (anamkatisha) …. Utaelewa je na akili zako finyu … hujalelewa kuthamini fikra nzito …
Tanzanite: aha! Unanikatisha kwa sababu huna hoja.
Uwe na subira. Nikueleze nafasi yangu. Viongozi wakisafiri ughaibuni mimi ndio wa kwanza kualikwa kuwasindikiza. Mimi sibebwi mgongoni. Ninawekwa mfukoni. Ninakutana na marais wa nchi kubwa; ninasalimiana na mafalme wa Uarabuni. Wanani papasa. Wananipenda.
Wewe … katika maisha yako yote hujakanyanga ardhi ya Ulaya wala Dubai. Ulichozoea ni kila mwaka kubebwa na vijana wakiimba:
Oo TANU yajenga nchi
Oo TANU ooo TANU ooo
Yajenga nchi ….
Eti mlikuwa mna jenga nchi? Nchi gani yenye barabara zilizojaa mashimo … Tazara yenu yenyewe ili hitaji vichwa viwili kuvuta mabehewa! Maduka yenu hayakuwa na colgati wala vipodozi kwa ajili ya wasichana warembo kama mimi.
Mwenge: sitaki kurudia kukudhalilisha. Sio staili yangu. Lakini ukweli unabaki pale pale. Huelewi kabisa dhana ya kujenga nchi. Umeenda shule, umesoma lakini hukuelimika. Hujui historia ya nchi yako.
Nyakati zile dhana ya kujenga nchi ilikuwa na maana ya kujenga utaifa. Tulipopata uhuru hatukuwa na Taifa, tulikuwa na makabila. Kizazi changu ndio kilichojenga Utanzania ambao mnaujivunia. Hata jina lako lenyewe ni Tanzanite – sio Chaagaite au Pareite au Sukumaite! Tuliwarithisha Tanzania. Bila sisi kujenga na kukuuza Utanzania mgekuta nchi yenu iko vipande vipande.
Tanzanite alibaki mdomo wazi … hakuwa na la kusema.
*****



Leave a reply to TheRoar Cancel reply